AMUUA MAMA YAKE MZAZI AKIDAI ‘AMEISHI KUPITA KIASI’

Baba mwenye watoto wanne amefikishwa mahakamani kujibu shtaka la kumuua mama yake mzazi mwenye umri wa miaka 89 akidai kuwa ameishi ‘kupita kiasi.’
Mtuhumiwa huyo, Satar ole Sanangi mwenye umri wa miaka 40, juzi alifikishwa mbele ya Hakimu Jesse Nyagah kwa tuhuma za kumuua mama yake mzazi, Kuyano Lesanangi.
Muendesha Mashtaka, Osman Mohammed alieleza Mahakama kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo Juni 14, 2017 baada ya kurejea nyumbani huku akiwa amelewa pombe na kwenda kwenye nyumba ya mama yake kufanya mauaji hayo.
“Mshtakiwa alikwenda moja kwa moja hadi ndani ya nyumba ya mama yake na alianza kumzomea kuwa hafai kuwa hai,” alisema muendesha mashtaka.
Alidai mshtakiwa alianza kuorodhesha majina ya waliokuwa rika moja na mama yake, lakini wote walikuwa tayari wamekwishafariki dunia.
“Mshtakiwa alimweleza mama yake kuwa hata yeye alikuwa anafaa kuondoka ulimwenguni ili aende waliko wakongwe wa rika lake,” aliendelea kusema muendesha mashtaka.
Muendesha mashtaka huyo alidai kuwa baada ya maneno hayo, mtuhumiwa alichukua fimbo na kumpiga mama yake na kusababisha kifo chake.
HT @ MWANANCHI

from Blogger http://ift.tt/2vrZHD2
via IFTTT