AFYA: LINDA MOYO WAKO UOKOE FIGO ZAKO

Na Dkt. Syriacus Buguzi Kila unapojisikia una afya njema usidhani kuwa utabaki kuwa hivyo siku zote ila inamaanisha kwamba kwa muda huo viungo vyako vya mwili vinafanya kazi vizuri na kwa uwiano unaotakiwa – hasa moyo na figo.
Mwenyezi Mungu Muumbaji aliumba miili yetu kwa namna ambayo figo na mfumo wa mzunguko wa damu ambao unahusisha moyo viwe vinategemeana kiutendaji kwa namna nyingi – hii yote ni kukufanya ujisikie katika afya nzuri wakati wote.
Lakini hatari ni kwamba kama kuna kitu hakitakuwa sawa kwenye moyo wako, figo nazo zinakuwa kwenye mashaka pia. Madhara ambayo figo zinaweza kuyapata kutokana na udhaifu kwenye moyo zinaweza zisionekane mapema – inachukua miaka mingi sana kwa madhara kuonekana.
Ukizingatia hili, itoshe tu kusema kwamba kama siku zote tukiwa tunahakikisha mioyo yetu inafanya kazi vizuri, basi jua kabisa kuwa na figo nazo zinakuwa zimeokolewa kutoka kwenye madhara ambayo mengine ni makubwa kama kushindwa kabisa kufanya kazi.
Ni kivipi shinikizo la juu la damu lina madhara kwenye figo?
Kimsingi, kiasi cha pili cha wingi wa damu mwilini mwa binadamu (asilimia 25) huwa inasukumwa kwenda kwenye figo kutoka kwenye moyo. Hii ni sawa na kiasi cha lita 1.1 kila dakika kwa mwanaume mtu mzima mwenye uzito wa kilo 70. Kiasi kikubwa huwa kinaenda kwenye ini (ambacho huwa ni asilimia 27.8)
Hata hivyo, uhusiano na muingiliano huu huu kati ya moyo na figo ni wa kulindwa sana kwakuwa ni rahisi kudhuriwa. Kwakuwa kazi ya figo ni kuchuja taka zilizopo kwenye damu, figo zinatumia mfumo mkubwa sana wa mishipa ya damu ili kufanya kazi hiyo kwa ufanisi uliokusudiwa, na hapa ndipo matatizo yanapoanzia.
Mishipa hii ya damu (inayotumiwa na figo) inaweza kupata madhara na kupasuka endapo moyo utakuwa unasukuma damu kwa wingi sana au kwa kasi kubwa kuliko uwezo wa mishipa hiyo kufanya kazi. Hii ndio sababu wagonjwa wengi wenye maradhi ya figo hapa Tanzania wanakutwa au wanakuwa na historia ya muda mrefu ya maradhi ya shinikizo la juu la damu (HBP). Tafiti zinaonesha kuwa Shinikizo la Juu la Damu ni sababu ya pili kwa ukubwa kwa matatizo ya figo.
Kwahiyo, kama ugonjwa wa shinikizo la juu la damu unabaki kwa muda mrefu bila kupatiwa suluhisho, itasababisha mishipa minene iliyopo nje ya figo yenye kazi ya kupokea damu inayotoka kwenye moyo kuminywa na kupungua unene, kudhoofu au kukakamaa.
Baada ya muda mrefu, mishipa ya damu midogo ambayo kazi yake ni kuchuja damu ndani ya figo kukosa hewa ya oksijeni na virutubisho vinavyotakiwa ili mishipa hiyo iweze kufanya kazi vizuri.
Jambo hili linasababisha madhara makubwa kwenye figo. Zinapoteza kabisa uwezo wa kuchuja damu, zinashindwa kudhibiti kiwango cha asidi na chumvi mwilini na mwisho kushindwa kabisa kufanya kazi.
Kwahiyo, hakikisha unapima moyo wako kujua kama unafanya kazi kama unavyotakiwa ili uweze kuokoa figo. Hakikisha unavijua vipimo hivi na maana yake kwakuwa ni kitu cha msingi sana kwa afya yako, na baada ya kuvijua uwe unafanya vipimo vya mara kwa mara ili uweze kuishi kwa afya njema wakati wote.

from Blogger http://ift.tt/2vrp6g1
via IFTTT