Madaktari bingwa watano watua njombe watatibu wagonjwa kwa siku tano

WIZARA ya afya, maendeleo ya jamii ,jinsia watoto na wazee, kupitia mfuko wa bima ya afya ya taifa NHIF imekabidhi madaktari bingwa watano wa magonjwa ya Moyo, Usingizi watoto na uzazi kwa wakina mama, katika hosptali ya mkoa wa Njombe kibena ambao watahudumu kwa siku tano.

Madaktari hao wameanza kutoa huduma ya afya kwa kushirikiana na wataalamu wa hospitali ya kibena mkoani Njombe kwa muda wa siku tano kwa kutibu magonjwa ya ndani ya moyo, usingizi (nusu kaputi) watoto na uzazi kwa akina mama.

Akiwakabidhi madaktari hao mkoani Njombe Mkurugenzi wa matibabu na huduma za kiufundi makao makuu NHIF Dr Frank Lekey alisema huduma hiyo kwa mkoa wa Njombe ni ya 16 na alikabidhi dawa na vitendanishi kwaajili ya kupimia magonjwa mbalimbali.

“Huduma hii tunaitoa mkoa wa Njombe ikiwa ni ya kumi na sita kutolewa hapa nchini na pia katika hospitali hii ya Kibena tunakabidhi dawa pamoja na Vitendanishi wa kupimia magonjwa mbalimbali hospitalini hapa” alisema Dr. Lekey.

Akizundua mpango huo kwa niaba ya katibu mkuu wa wizara ya afya Dr. Mpoki Ulisubisya, mganga mkuu wa Hospitali nchini Prof. Mohamed Bakari alieleza dhamira ya wizara na mfuko kuwa ni kuifikia jamii kubwa kwa urahisi kwa kuwasogezea Madaktari katika ngazi ya mkoa.

Prof. Bakari pia alitoa wito kwa wananchi kujiunga kwa wingi na mfuko huo wa afya ili kuendelea kupata huduma za afya bure pindi wanapo ugua kuriko wakisubili kulipia wakiwa wanaumwa.

“Wananchi jiungeni na mifuko ya bima ya afya kwa kuwa katika mifuko hii mnawekeza pesa kwaajili ya kutibiwa ukiugua kwa kuwa ugonjwa hauchagui sasa una pesa ama hauna kwa hiyo unaweza kuugua wakati hauna pesa na ukashindwa kununua dawa” aliongeza Prof. Bakari.


Aidha NHIF Imekabidhi dawa na vitendanishi kwa hospitali hiyo vyenye thamani ya shilingi milioni tano ambapo mganga mkuu wa mkoa wa Njombe Dr Samweli Mgema akitumia fursa hiyo kuushukuru mfuko wa bima ya afya NHIF kwa kuwapatia dawa hizo.


Kwa upande wao wananchi wa Mkoa wa Njombe wameishukuru serikali kupitia NHIF kwa  Kusogeza huduma hiyo ya madaktari bingwa ambayo kabla wamekuwa wakiipata nje ya mkoa tena kwa gharama kubwa na kuwa wamekuwa wakilazimika kwenda jijini Dar Kwaajili ya kutibia magonjwa ya moyo.