Siku za mwisho za Mtikila.

Mchungaji Christopher Mtikila.
Mchungaji Christopher Mtikila, ambaye ni Mwenyekiti wa Democratic Party (DP), amefariki dunia baada ya gari lake alilokuwa akisafiria kupinduka eneo la Msolwa, Chalinze Wilaya ya Bagamoyo mkoani Pwani.
 
Kufikia jana asubuhi wakati taarifa za kifo cha Mtikila zikisambazwa kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, tayari Mchungaji huyo wa Kanisa la Salvation Army, alishafichua jambo zito alilokuwa nalo moyoni kuhusiana na uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 25, mwaka huu. Alifariki dunia baada ya gari alilokuwa akisafiria aina ya Toyota Corolla, T 189 AGM, kuacha njia na kupinduka saa 11:45 alfajiri jana.
 
Mtikila alifichua ya moyoni siku moja kabla ya kifo chake wakati akizungumza na wananchi waliojitokeza kwenye mkutano wa kampeni wa mgombea ubunge wa chama chake Jimbo la Njombe Kusini, William Myegeta.
 
Katika mkutano huo uliofanyika kwenye viwanja vya National Housing mjini Njombe, Mtikila aliwaambia wananchi kuwa anaamini atashinda rufaa dhidi ya kuenguliwa kwake na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kugombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa sababu hiyo, aliwataka Watanzania wasijisumbue kufikiria kuwapigia kura wagombea wa vyama vingine kwani hawana sifa na badala yake, wajiandae kumchagua yeye ili awe kinara wa ukombozi wa kweli wa Tanzania.   
 
Mtikila alisema kuwa ukiondoa yeye ambaye ana uhakika atarudishwa kugombea licha ya Nec kumuengua kutokana na kasoro zilizodaiwa kufanywa na mgombea mwenza wake, wagombea wote kutoka vyama vingine hawana sifa, wakiwamo Dk. John Magufuli anayepeperusha bendera ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Edward Lowassa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayewakilisha pia vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya NCCR-Mageuzi, NLD na Chama cha Wananchi (CUF).
 
“Wote waliosimamishwa kutaka kutuongoza hawataikomboa nchi yetu. Mniombee nifanikiwe rufaa yangu na nishinde... vinginevyo msipige kura ya urais. Pigeni kura za wabunge ambao mnawaamini ili baadaye uchaguzi urudiwe na mimi nikichukua fomu nina imani lazima nitashinda tu,” alisema marehemu Mtikila, siku moja kabla ya kifo chake.
 
Alisisitiza kuwa kwa namna yoyote ile, akishashinda rufaa yake siku ya uchaguzi itaahirishwa ili kutoa nafasi kwa yeye na chama chake kuwamo kwenye kinyang’anyiro hicho na hivyo, akawataka wajiandae kuwapigia kura wabunge na madiwani na kwamba, siku itakayopangwa kwa uchaguzi wa rais, yeye apigiwe kura nyingi ili asjinde kwa klishindo na kuleta ukombozi wa kweli kwa Watanganyika.
 
Kadhalika, Mtikila alizungumzia umuhimu wa kupimwa afya kwa kila mgombea wa nafasi ya urais kwani kufanya hivyo, ni utaratibu ulizoeleka kwa kila kazi inayoombwa na mtu na jambo hilo ni kwa manufaa ya taifa.
 
“Kazi yoyote unayoomba huwa ni lazima uende hospitalini kuchunguzwa afya kwa kuwa mtu ukiwa na ugonjwa wowote mwilini mwako huwezi kuongoza vizuri,” alisema. Aidha, alidai kuwa yeye hajazi watu katika mikutano yake kwa kuwa hawanunulii pombe aina ya viroba, lakini anaamini Watanzania waliopo katika mkutano wake wa Njombe ndiyo watakaosambaza taarifa za ukombozi kwa wale ambao hawakubahatika kuhudhuria mkutano huo.
 
Alisema mbali na kumpigia kampeni ubunge wa chama chake katika Jimbo la Njombe Kusini, pia atazunguka nchi nzima kufanya kazi hiyo kwani wamesimamisha wagombea wengi wa nafasi ya ubunge na udiwani, karibu katika kila upande wa nchi.
 
POLISI WAZUNGUMZIA AJALI 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Ibrahim Jafarry, alisema gari alilokuwa akisafiria Mtikila lilikuwa katika mwendo wa kasi kubwa na kwamba baada ya kufika katika eneo la ajali liliacha njia na kupinduka. Alisema Mtikila alikuwa na abiria wengine wawili ndani ya gari hiyo pamoja na dereva. 
 
Hata hivyo, alisema wenzake wote walijeruhiwa na kukimbiziwa katika Hospitali Teule ya Tumbi, Kibaha. Kamanda Ibrahim aliwataja majeruhi kuwa ni dereva George Steven maarufu kama Ponera (31), mkazi wa Mbezi jijini Dar es Salaam na abiria wengine ni Mchungaji Patrick Mgaya (57), mkazi wa Dar es Salaam na Ally Mohamed (42), mkazi wa Mbezi Dar es Salaam.
 
Ilielezwa zaidi kuwa Mchungaji Mtikila alianza safari kutokea Njombe juzi saa 3:00 usiku baada ya kumalizika kwa mkutano wa kampeni.
 
Wakati huo huo, Mganga Mkuu wa Hospitali Teule ya Tumbi, Dk. Peter Dastan, aliiambia Nipashe kuwa hadi kufikia jana alasiri walikuwa bado wakiufanyia uchunguzi zaidi mwili wa marehemu Mtikila ili kubaini kwa kina sababu za kifo chake.
 
ENEO LA AJALI
Katika hatua nyingine, Kamanda Ibrahim alieleza kuwa kabla ya kifo chake, Mtikila alikuwa amekaa katika kiti cha mbele na kwamba gari hilo alilokuwa akisafiria halionyeshi kuwa ni la kwake bali alilikodi na mmiliki wake ni mkazi wa jijini Dar es Salaam.
 
Taarifa zaidi zimeeleza kuwa eneo la Msolwa alilopata ajali Mchungaji Mtikila na kufariki dunia siyo mara ya kwanza kushuhudiwa ajali mbaya kama ya jana na kusababisha vifo au majeruhi. 
 
Taarifa iliyothibitishwa na Kamanda Ibrahim ilieleza kuwa Februari 2013, eneo hilo liliwahi kukumbwa na ajali iliyohusisha vifo vya wanafunzi watatu wa shule ya sekondari na raia wengine waliokuwa wameomba msaada wa ‘lifti’ kwenye gari dogo aina ya Toyota Mark II kabla gari hilo lililowapakia kugongana uso kwa uso na lori aina ya Fuso na kusababisha vifo vya wanafunzi hao.
 
SALAMU ZA RAMBIRAMBI
Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazelendo, Samson Mwigamba, alisema wamepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Mchungaji Mtikila kwani anaamini kuwa mchango wake ulikuwa unahitajika zaidi sasa katika wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu.
 
Mgombea ubunge wa DP Jimbo la Njombe Kusini, William Myegeta, amesema amepokea kwa masikitiko makubwa msiba huo na kuwa Chama na Taifa vimempoteza mtu muhimu kisiasa.
 
Katibu Mwenezi Taifa wa DP, Msambichaka Feruz, alisema chama kimepata pigo kwa kuondokewa na Mchungaji Mtikila na kwamba mambo yote aliyokuwa akiyapigania yataendelezwa.
 
Katibu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe, alisema kuwa chama chake kitamkumbuka Mchungaji Mtikila kutokana na harakati zake za mageuzi nchini tangu miaka ya 1990.
 
Mwenyekiti wa Chama cha Kijamii (CCK), Costantine Akitanda, alisema kuwa taifa limempoteza mzalendo wa kweli aliyesimamia kauli zake bila ya woga.
 
Alisema, marehemu Mchungaji Mtikila alikuwa na misimamo isiyoyumba hata pale wengine walipompinga na aliweza kuwasemea vyema Watanzania wenzako na kuonyesha uzalendo wa kweli.
 
Jana, majonzi yalitawala nyumbani kwa marehemu Mtikila, eneo la Mikocheni B jijini Dar es Salaam. 
 
Viongozi na watu kadhaa walionekana wakiwa na huzuni kubwa kutokana na taarifa za kifo cha kiongozi huyo.
 
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alisema amepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa taarifa za kifo cha Mchungaji Mtikila.
 
Mbowe alisema kifo cha Mchungaji Mtikila kimeacha pengo kubwa katika siasa za mageuzi nchini hasa katika kupigania Tanganyika na suala la mgombea huru kuwa haki ya kikatiba nchini.
 
lImeandikwa na Magreth Malisa, Yasmine Protace, Furaha Eliab na Christina Mwakangale na Thobias Mwanakatwa.
SOURCE: NIPASHE