Mtikila: Mwanasiasa mtata atangulia.


Mchungaji Christopher Mtikila.
Christopher Mtikila, Mchungaji wa Kanisa la Salvation Army pia mwanasiasa wa mageuzi nchini hatunaye tena. Mwanasiasa huyo machachari ana historia ndefu, yenye sura ya kukanganya. Jina la Mtikila lilianza kutikisa vichwa vya vyombo vya habari mwanzoni mwa miaka ya 90 wakati harakati za mageuzi zimepamba moto nchini.
 
Mtikila ambaye alifariki dunia jana katika ajali ya gari eneo la Msolwa, Chalinze mkoani Pwani, alikuwa ni miongoni mwa wajumbe wa awali wa kamati ya kuratibu mageuzi nchini iliyoanzishwa Januari 1991 ikijumuisha watu mbalimbali waliokuwa wamejitokeza kuongeza shinikizo la kutaka Tanzania irejee kwenye mfumo wa vyama vingi. 
 
Kamati hii ilikuwa na jina la National Committee for Constitutional Reform (NCCR), ilijumuisha wanasiasa, wasomi na wanaharakati mbalimbali waliokuwa wameamua kujitoa mhanga kuona kwamba Tanzania inapata mfumo wa vyama vingi. Hata hivyo, NCCR hiyo haikudumu sana kutokana na tofauti za kimitazamo miongoni mwa wajumbe wake, hali hiyo ilisababisha wajumbe wa kamati hiyo kujiengua na kuanzisha vyama vyao vya siasa.
 
Miongoni mwa kundi lililounda NCCR ni pamoja na Mtikila, kina Mabere Marando, Balozi Kasanga Tumbo, James Mapalala na wengineo. Kwa maneno machache tunampomzungumzia Mtikila leo, tunamzungumzia mwanasiasa ambaye alishiriki mageuzi ya miaka ya 90, lakini kwa mawazo yaliotofautiana sana na wenzake.
 
Ni Mtikila ambaye aliibuka na msimamo kwamba jambo la kwanza kabisa kabla ya kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini, hatua ya kwanza ilipaswa kuwa ni kuandikwa kwa katiba mpya. 
 
Msimamo huo wa Mtikila juu ya katiba kwanza kabla ya uchaguzi wowote ulimfarakanisha na wanasiasa wenzake na hasa ikikumbukwa kwamba chama chake cha Democratic Party (DP) kilikuwa na falsafa moja kubwa, kwamba Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ulikuwa ni batili, kililaani kwa nguvu zake zote utawala wa Rais Ali Hassan Mwinyi (Mzee Ruksa) kwamba haukuwa halali kwa Watanganyika kwa kile alichodai ni sawa na kuvunja maagizo ya Mungu kwamba ‘si halali kumtawaza mgeni kuwa mfalme nyumbani kwako.’
 
Mtikila alikuwa na uwezo mkubwa wa kuzungumza, alijua kujenga hoja, hotuba za kisiasa alizichanganya na maagizo ya Mungu kutoka kwenye kitabu cha waumini wa Kikristo Biblia. Kuibuka kwa Mtikila kulishangiliwa sana na makundi ya vijana wakati huo.
 
Wakati mageuzi yakianza kupamba moto, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwanzoni mwa miaka ya 90 kilikuwa ni kitovu cha mijadala ya mageuzi. Ni katika kipindi ambacho Idara Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma katika kilichokuwa kitivo cha Sanaa na Sayansi ya Jamii (FASS), kilikuwa kinaalika wenyeviti wa vyama mbalimbali vya siasa vilivyokuwa vimeanzishwa.
 
Pamoja na wenyeviti wengi walioalikwa, pia Mchungaji Mtikila alifika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika mlolongo wa semina za wanasiasa kuzungumza na jamii ya wasomi ya chuo kikuu kueleza chama chake cha DP kilikuwa kinasimamia nini.
 
Ninakumbuka wahadhiri wa Idara Sayansi ya Siasa na Utawala wa Umma walikuwa wamepeana zamu za kuwa waratibu wa mijadala katika semina hizo.
 
Wakati huo, tofauti na ilivyo sasa lugha iliyokuwa inatumika katika mikutano hiyo ilikuwa ni lazima iwe Kiingereza. Hofu kuu iliyokuwa miongoni mwa wanafunzi ni kwamba hivi kweli Mtikila alikuwa na uwezo wa kuhimili lugha hiyo mbele ya wanataaluma waliobobea katika ukumbi wa Nkrumah? 
 
Wengi wa wanafunzi ilikuwa ni siku yao ya kwanza kukutana ana kwa ana na Mtikila, kilichotokea ukumbini siku hiyo ilikuwa ni maajabu. Nakumbuka siku hiyo kiongozi wa mjadala alikuwa Dk. Charles Gasarase, akiwa mhadhiri mwandamizi kutoka idarani humo. Kabla ya Mtikila kuzungumza Dk. Gasarase alitoa angalizo kwa Mtikila, kwamba hadhira iliyokuwa mbele yake ni ya wasomi ambao maisha yao yanaendeshwa kwa kusimama kwenye ukweli halisi wa mambo (facts). Alimkumbusha Mtikila kwamba chochote atakachosema ni lazima kujikite katika msingi huo.
 
Aliposimama Mtikila alibadilisha hali ya hewa kwenye ukumbi huo, kwani siyo tu aligeuza angalizo la Dk. Gasarase kuwa halina maana kwa kile alichosema kuwa katika maisha yake hachaguiwasomi au walalahoi, hachangui kundi lolote, anachokijua yeye ni kusema ukweli na ni ukweli alikuwa amedhamiria kuusema. Katika kutoa ufafanuzi huo, Mtikila alikuwa anatiririka kwa lugha ya Kiingereza safi kilichonyooka na kilichojaa misamiati mizito. Matokeo yake, umati wa wanafunzi waliokuwa wamefurika ukumbi wa Nkrumah walilipuka kwa nderemo na vifijo.
 
Kilichotokea Chulo Kikuu cha Dar es Salama siku hiyo baada ya Mtikila kuzungumza ni historia, kwani kati ya wanasiasa wa vyama vyote waliokuwa wamefika chuo hapo (zaidi ya vyama vitano), hakuna ambaye gari lake lilisukumwa. Gari la Mtikila lilisukumwa kuanzia maeneo ya Utawala hadi karibu na Chuo cha Maji, Ubungo. Zungumza ya Mtikila iliwajengea hamasa kubwa wanafunzi siku hiyo.
 
MTIKILA NA GABACHOLI NA WALALAHOI
Katika kipindi cha miaka ya mwanzo ya 90 pia viwanja wa Jangwani viligeuka kuwa kitovu cha mikutano ya wanamageuzi. Vyama vingi vipya vilivyokuwa vimeanzishwa viliendesha mikutano ya kujitangaza katika viwanja hivyo.
 
Katika moja ya mikutano iliyofanyika Jangwani ilikiwa siku ya Jumamosi, Mtikila alikuwa msemaji mkuu wa chama chake. Ni katika mkutano aliotumia majina ya ‘Gabacholi na Walalahoi’ na jinsi nchi inavyoibiwa na kuporwa na wageni. Mtikila alikuwa na lugha ya kuhamasisha, alijua kujieleza, alijua kujenga hoja, baada ya hotuba yake Jangwani siku hiyo, vijana kwa mamia walimiminika mitaa ya Kariakoo na kuanza kuvamia maduka, wakionyesha kuamshwa na hotuba ya Mtikila. 
 
Ni kipindi ambacho Mtikila alikuwa ni mteja wa kudumu wa sero za Polisi. Ni kipindi ambacho Mtikila alikuwa anasababisha mabomu ya machozi ya polisi kurindima mitaani kila alipomaliza mikutano yake. Ni kupindi ambacho kauli za kuonyesha jinsi wananchi walivyotaabika kutokana na mfumo mbovu wa utawala usiowajali zilitamba na kuasisi majina ya walalahoi na magabacholi.
 
Baada kuridhiwa kwa mfumo wa vyama vingi uliotokana na ripoti ya Tume ya Jaji Nyalali, Mtikila alisajili chama cha DP, lakini akiwa ameapa kwamba asingekwenda Zanzibar kutafuta wanachama kama sheria ya vyama vya siasa ya mwaka 1992 inavyoelekeza, akisisitiza kwamba kwake Zanzibar ni nchi ya nje. 
 
Msimamo huu ulimfanya Mtikila kukosa usajili wa kudumu wa chama chake kwa muda mrefu. Katika kipindi ambacho anasaka usajili, alianzisha Dawati la Uhuru (Liberty Desk). Ni kupitia dawati hili Mtikila alikuwa anajirekodi kwenye kanda za kaseti (audio) na kuzisambaza akiwa anazipachika salama za Saa ya Ukombozi ni Sasa’. Mara kadhaa polisi walimkamata Mtikila na kanda hizi na kumfungulia mashitaka.
 
Mengi aliyashinda, na kurejea uraiani na kuendelea na mapambano huku nyumbani kwake akipeperusha bendera ya Tanganyika.
 
MTIKLA NA MGOMBEA BINAFSI
Kama kuna sehemu Mtikila alikuwa hakosekani ni mahakamani. Alizijua korido za mahakama za Tanzania. Alizijua ama akiwa anashitakiwa na Jamhuri au yeye binafsi akiwa amefungua mashitaka dhidi ya Jamhuri akipigania suala la mgombea binafsi. Mtikila alifungua kesi kadha za kikatiba.
 
Miongoni mwa kesi hizo ni ile iliyotolewa hukumu na Jaji wa Mahakama Kuu mkoani Dodoma,  Kahwa Lugakingira, juu ya mgombea binafsi. Kwa mara ya kwanza, Mchungaji Mtikila, alifungua kesi ya kikatiba mwaka 1993 katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dodoma, akitaka kuruhusiwa kwa wagombea binafsi katika chaguzi kwa maelezo kuwa haki ya kuchagua na kuchaguliwa ni ya msingi na imeainishwa katika katiba.
 
Katika uamuzi wake, Marehemu Jaji Kahwa Lugakingira, alikubaliana na hoja za Mtikila na kuitaka serikali kuwaruhusu wagombea binafsi kwa kuwa ni moja ya haki za msingi za binadamu za kiraia na kisiasa.
 
Hata hivyo, licha ya mahakama kukubaliana na hoja za Mtikila, serikali haikukubaliana na uamuzi huo, badala yake mwaka 1995, iliandaa muswada wa sheria na kuuwasilisha bungeni, ukipinga kuwapo kwa wagombea binafsi.
 
Muswada huo ulipendekeza kwamba mgombea yeyote wa nafasi ya kisiasa kuanzia serikali za mitaa, udiwani, ubunge na urais sharti apitie kwenye vyama vya siasa.
 
Hatua hiyo ndiyo iliyomlazimisha Mchungaji Mtikila kufungua kesi nyingine ya kikatiba Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam na kushinda tena katika uamuzi uliotolewa na  Jaji Amir Manento, Salum Massati na Thomas Mihayo. Serikali haikukubaliana na hukumu hiyo ndipo ilikata rufaa na kufanikiwa kuipangua baada ya jopo la majaji saba wa Mahakama ya Rufani kuitengua. Mtikila hakuishia hapo, alikwenda hadi Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu kutafuta haki hiyo, aliipata mwaka jana, lakini hadi mauti yanamkuta serikali imegoma kuruhusu mgombea binafsi na hata uchaguzi mkuu unaoendelea sasa hakuna mgombea binafsi.
 
MTIKILA NA SIASA TATA
Mchungaji Mtikila alipita katika mapito magumu. Atakumbukwa kuwa ni mwanasiasa wa kizazi cha sasa ambaye alifungwa jela mwaka mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la uchochezi. Kwa wastani Jamhuri ilikwisha mfungulia Mtikila kesi 43 kwa mujibu wa kauli yake mwenyewe mahakamani wakati akijitetea dhidi ya kesi ya uchochezi/jinai namba.132/2010 aliyoshitakiwa kwa kudai kuwa Rais Jakaya Kikwete alikuwa na mpango wa kuumaliza Ukristo Tanzania. 
 
Katika mlolongo huo ni kesi moja tu alitiwa hatiani ya kutoa maneno ya uchochezi akiituhumu CCM, kuwa ilimuua aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Horace Korimba. 
 
Hakimu wa mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Stella Mwandu, alimfunga mwaka mmoja jela.
Mbali na kesi hizi, Mtikila alikuwa na hulka ya kuibuka na kutoa madai mazito dhidi ya watu mbalimbali. 
 
 Miongoni mwake ni ile aliyotoa wilayani Tarime wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge kuwa waliomuua Chacha Wangwe ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, kauli hiyo ilimfanya ashambuliwe kwa mawe na kujeruhiwa kichwani. 
 
Yapo mengi kuhusu utata wa Mtikila, kwa leo itoshe tu kusema kuwa Tanzania imempoteza mwanasiasa asiyetabirika, aliyepitia mengi, aliyeibua changamoto na mijadala mingi. Pamoja na yote haya, ametangulia mbele ya haki. Mungu ampe pumziko la amani.
 
BY JESSE KWAYU

SOURCE: NIPASHE