Lowassa akerwa wafuasi wake kupigwa mabomu.


Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha 
Demokrasia na Maendeleo (Chadema)
 anayeungwa mkono pia na Umoja wa 
Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa.
Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anayeungwa mkono pia na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa, ameelezea kusikitishwa na hatua ya polisi jijini Tanga kuwapiga mabomu wananchi waliokuwa wakirejea makwao kutoka katika mkutano wake wa kampeni juzi.

“Niliporejea hotelini baada ya mkutano jana (juzi), nilipata taarifa kwamba polisi waliwapiga mabomu wafuasi wa Ukawa, nasikitika sana kwa kitendo kile, kwa sababu tulikubaliana polisi wasipige watu mabomu,” alisema akiwataka washirikiane na polisi kufanya kazi pamoja.

Aliyasema hayo alipokuwa akizungumza naumati wa wakazi mji wa Korogwe katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Korogwe jana.

Kuhusu hali ya kiuchumi ya Mkoa wa Tanga, Lowassa alisema atachukua maamuzi magumu ya kufumua na kujenga Bandari ya Tanga na kufufua reli. Alisema serikali atakayoiunda na kuiendesha kwa mwendo kasi wa kilomita 120 kwa saa, itatatua matatizo hayo yote ya Mkoa wa Tanga na kama kuna atakayeshindwa kuhimili kasi hiyo, basi hana budi kujiondoa.

Aidha, alizungumzia tatizo la mashamba pori ambalo ni sugu mkoani Tanga, akisema atamaliza tatizo hilo akipewa ridhaa ya kuwa Rais. “Tatizo la mashamba pori hapa Tanga ni kubwa sana, kwa nini tusimalize tatizo hilo,” alisema.