TAJIRI AFA, MALI ZAZUA BALAA

ALI za aliyekuwa tajiri maarufu Dar, marehemu Charles John Mallya zimezua balaa baada ya mke mkubwa, Philomena Masechu ambaye anadai kuchuma naye kiasi kikubwa cha mali hizo kusema amedhulumiwa na mke mdogo, akimtaja Mariana kwa kushirikiana na watoto wa wake wengine wa marehemu.


Marehemu Charles John Mallya enzi za uhai wake.

Akizungumza na gazeti hili kwa masikitiko, Philomena alisema uchochezi mkubwa ulifanywa na watoto wa nyumba zingine ndogo (wake wenzake).“Tangu ujana tulihangaika na marehemu na kufanikiwa kupata mali nyingi, nikiwa kama mshauri wake lakini sasa watoto wa wake zake wengine wawili waliyokuwa katika mikono yangu wamefikia hatua ya kunidhulumu kila kitu. Hivi sasa naishi kwenye kijumba kidogo nilichojengewa na ndugu zangu,” alisema mwanamke huyo huku akilia.

Philomena aliendelea kusema kuwa, hitaji lake kubwa ni kupewa nyumba moja ya ghorofa iliyoko Sinza na nyumba ambayo haijaisha iliyoko Moshi, Kilimanjoro.Naye mmoja wa watoto wa mama huyo, Brighton Mallya akisimulia hali hiyo, alisema: “Baba aliacha mali nyingi na kutamka kuwa ni aseti ambayo kila mtu akipata shida ataweza kutatuliwa kupitia mali hizo kwa utaratibu na makubaliano, lakini sasa zimetekwa na baadhi ya ndugu.”

Kwa mujibu wa nyaraka zenye mali za marehemu Mallya, sehemu ya mali alizoziacha ni kampuni ilitwayo Mti Mmoja Enterprises, jina linalotumika katika baadhi ya miradi. Pia aliacha maduka 2, mashamba, biashara ya magari, viwanja zaidi ya 4, nyumba za kawaida, nyumba 3 za biashara ambazo ni ghorofa (zina vyumba 105) pia kuna nyumba zingine za biashara ikiwemo Mariana Bar, Mti Mmoja Annex na Mti Mmoja Guest ambazo ziko Sinza Mugabe, Dar.


Baadhi ya mali alizoacha marehemu.

Aidha, kwa mujibu wa nyaraka hizo thamani ya mali hizo ni zaidi ya shilingi bilioni moja na milioni mia tano (kwa mwaka 2010) ambapo walalamikaji hao wanasema ilitakiwa kila mtu apate haki yake kama inavyostahili na kusingekuwa na malalamiko.

Baada ya kupata tuhuma hizo timu ya Uwazi iliamua kumtafuta mke huyo mdogo ambapo aliposomewa mashtaka aliliambia Uwazi:“Siwezi kuzungumza, naumwa, ongea na mtoto wangu.”
Akampa simu mwanaye wa kiume ambaye aliposomewa madai ya Philomena, alijibu: Iwe mwanzo na mwisho kupiga simu hii.”

Uwazi lilipohitaji ufafanunuzi zaidi alijibu yeye si mwalimu wa kufafanua.
Dawati letu lilifanikiwa kupata baadhi ya nyaraka zinazoonesha marehemu Mallya alizaliwa mwaka 1934, mwaka 1959 alioa mke mkubwa (Philomena) na walifanikiwa kupata watoto 6 na kuwa na biashara ya bar na hotel mjini Moshi.
Mwaka 1956 alimuoa Salome Gasper wakajaliwa kupata watoto wanne.

Mwaka 1963 alimuoa Joyce Mowo na kufanikiwa kupata naye mtoto mmoja. Mwaka 1977, Solome aliaga dunia na mwaka huohuo alimuoa Mariana ambapo mwaka 2010, mwezi Machi, ndipo mzee huyo alikumbwa na mauti kwa maradhi ambayo hayakutajwa