STARS WAFIKA GAMBIA HOI BAADA YA SAFARI YA NDEGE, BASI NA BOTI

Na Prince Akbar, Banjul, Gambia,
KIKOSI cha timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, kimewasili mjini Banjul, Gambia jana saa 11 jioni baada ya msoto wa safari ya ndege kutoka Dar es Salaam hadi Senegal, basi hadi mpakani mwa nchi hizo na kuvuka kwa boti kuingia mjini humo tayari kwa mechi ya kufuzu Kombe la Dunia kesho dhidi ya wenyeji.
Stars baada ya kufika Senegal hawakupata ndege ya kuunganisha kwenda Gambia, ikawabidi wasafiri kwa basi kwa muda wa saa sita barabarani hadi mpakani mwa Senegal na Gambia.
Wachezaji Stars wakiwa uwanja wa ndege wa Dakar, Senagal wakisubiri basi kuelekea mpakani mwa Gambia


Mrisho Ngassa amesema hajawahi kusafiri safari ngumu kama hiyo

Vijana hoi

Baada ya kufika mpakani hapo, wakatembea kwa miguu nusu saa hadi kwenye pantoni, ambako walipanda na kufika Banjul saa 11 jioni, moja kwa moja kufikika vitandani.
Stars imefikia katika hoteli ya Sea View Garden na leo inatarajiwa kufanya mazoezi mepesi kabla ya mechi kesho.
Mshambuliaji tegemeo wa Stars, Mrisho Khalfan Ngassa alisema hajawahi kusafiri safari ngumu kama hiyo maishani mwake na amechoka kupita kiasi.
Kwa ujumla wachezaji wa Stars wamefika Banjul wakiwa hoi na dhahiri mchezo wa kesho utakuwa mgumu kwao. 
Stars na Gambia zote zinacheza mechi ya kesho kukamilisha ratiba, kwani hazina tena nafasi ya kufuzu Kombe la Dunia mwakani nchini Brazil, baada ya kuzidiwa kete na Ivory Coast, ambayo kesho itamaliza na Morocco, timu nyingine katika kundi hilo. 
Lakini kocha Kim Poulsen amesema anataka kuutumia mchezo kushinda ili kushika nafasi ya pili katika kundi lake- ili kutengeneza mazingira ya kupanda kwenye viwango ya FIFA.