Kosa Kubwa Ambalo Waajiriwa Wengi Wanafanya Na Linawazuia Kufanikiwa (Kama Umeajiriwa Usiache Kusoma Hapa).

Kuna njia tano halali za kutengeneza kipato na hata kufikia mafanikio ya kifedha, yaani utajiri. Njia ya kwanza kabisa kwenye njia hizi ni ajira, lakini kama utakuwa makini sana kwenye ajira hiyo. Njia nyingine ni kuanzisha biashara yako, kuwekeza kwenye mali(majengo na ardhi), kuwekeza kwenye hisa na njia ya tano ni kutumia mtandao wa intaneti.
Hapa kwenye AMKA MTANZANIA tumekuwa tunazungumzia njia zote hizi tano kwa undani sana. Kufanikiwa kwenye kazi tumezungumzia hapa, fungua kusoma makala hizo. Kuhusu biashara na ujasiriamali tumejadili sana hapa, fungua pia usome, uwekezaji kwenye mali nako tumejadili sana, fungua hapa usome na kutengeneza fedha kwa njia ya mtandao, kuna kitabu kabisa, fungua hapa kukipata.
Leo nataka tujadili kuhusu njia ya kwanza kabisa ambayo ni ajira.
HATA KAMA UMEAJIRIWA, IMILIKI KAZI YAKO.
 
Kwanza kabla hatujafika mbali, naomba tukubaliane jambo moja, sio kila mtu anaweza kuwa mjasiriamali, au kuanzisha biashara yake mwenyewe. Kuna watu ni wataalamu wazuri sana na wanataka kupeleka nguvu zao kufanya kazi ambayo wanaona ni muhimu sana kwao. Watu wa aina hii hawawezi kuendana na mikiki mikiki ya kuendesha biashara. Kuna watu wengi ambao ni wafanyakazi wazuri na wanataka wakilala usiku walale kwa amani wakijua kesho wanaamka na kwenda kufanya kazi zao vizuri, na sio kukosa usingizi kwa kufikiria fedha ya kulipa watu inatoka wapi(kama umewahi kuendesha biashara utakuwa unajua ni nini nasema hapo).
Kwa hiyo kwa hayo basi, kuna watu wanachagua kuwa wafanyakazi, na wanajitoa kweli kwenye kazi zao. Tunaweza kuwaita watu hawa WAJASIRIAKAZI. Swali linakuja kwa nini wafanyakazi wengi wanaonekana kuwa na maisha magumu? Maisha ya kutegemea mshahara na kuishi kwa madeni? Hizi ni changamoto kubwa ambazo tutaendelea kuzungumzia moja moja kadiri tunavyokwenda.
Leo tunazungumzia mafanikio kupitia kazi, je inawezekana mfanyakazi akafanikiwa kwa kuendelea kuwepo kwenye ajira? Na kama ndio kwa nini wengi hawafanikiwi?
Ndio inawezekana kabisa mtu akafanikiwa kupitia ajira na wengi hawafanikiwi kwa sababu kuna kosa moja kubwa sana wanalolifanya kwenye ajira zao. Na kosa hili limekuwa sumu kubwa sana kwenye ukuaji wao na mafanikio yao kupitia kile wanachofanya. Naomba niweke wazi kwamba mafanikio ninayozungumzia hapa sio ya kifedha tu, bali mafanikio kwa ujumla, ikiwepo kuridhishwa na kazi unayofanya, kutoa mchango chanya kwa wengine, kuwa na maisha yenye furaha na hata mahusiano mazuri na wengine na kuwa na uhuru wa kifedha.
Sasa wafanyakazi wengi wamekuwa kama wafungwa ndani ya kazi zao, hawaoni kazi hizo zikiwafikisha popote zaidi ya kuendesha tu maisha yao ya kila siku, kazi zimekuwa mateso kwao na hata wakifikiria kuacha, bado mbele wanaona giza. Kama umefika kwenye hatua hiyo, endelea kusoma, dawa ya hali hii ipo mbele kidogo tu, ukianza kuitumia utaona mabadiliko makubwa kwako na kwa kazi yako.
SOMA; Kitu Kimoja Kitakachoongeza Wasifu Wako(Cv) Na Kukuongezea Kipato Pia.
Ni kosa gani ambalo wafanyakazi wamekuwa wakifanya?
Kosa moja kubwa sana linawazuia wafanyakazi kufurahia kazi zao na hata kufikia mafanikio makubwa, kosa hilo ni KUFIKIRI KWAMBA WANAMFANYIA MTU MWINGINE KAZI. 
Ukweli ni kwamba hata kama umeajiriwa na unafanya kazi ambayo umepangiwa na mwajiri wako, ile kazi unayofanya humfanyii mwajiri wako, bali unajifanyia wewe mwenyewe. Japokuwa umeajiriwa, lakini ukweli unaotakiwa kujua ni kwamba umejiajiri mwenyewe. Japokuwa mwajiri wako ndio anayeamua mshahara wako, ukweli ni kwamba wewe mwenyewe ndio unaamua ni mshahara kiasi gani mwajiri akupe. Kwa kifupi wewe upo kwenye ajira, ila unajifanyia kazi mwenyewe, umejiajiri mwenyewe, na unaamua ni kiasi gani cha mshahara ulipwe.
Ndio hivyo tu, ukiweza kujua kitu hiko kimoja na ukafanyia kazi kama nitakavyokufafanulia hapo chini, umeshategua kitendawili na hakuna kitakachokuzuia kufikia mafanikio kupitia ajira yako.
Japokuwa umeajiriwa, umejiajiri mwenyewe.
Japokuwa upo kwenye ajira, lakini kazi unayofanya itasimama kwa jina lako mwenyewe. Kama utafanya kazi bora sana, kila mtu atajua kuhusu wewe, utaongeza thamani ya sehemu yako ya kazi na utakuwa mtu muhimu sana. Huwezi kufanya hivi kama unafikiri kazi unayofanya siyo ya kwako. Kama unasubiri usukumwe kufanya majukumu yako. Kama unakazana kukwepa majukumu yako. Kama unafanya kazi ili uonekane upo bize wakati unajua kabisa hakuna kikubwa unachofanya. Ni kama kuinama kwenye kompyuta kwa makini, kumbe unacheza karata, kwa sababu kompyuta imempa mgongo anayekuja, watu wanaweza kufikiri upo na kazi kubwa kumbe hakuna lolote.
Kama unaingia kazini kwa kuchelewa na unaondoka kwa kuwahi huwezi kabisa kufikia mafanikio tunayosema hapa. Kama jumatatu unaanza kwa kisirani na kusema ni BULE MONDAY na ijumaa unaikaribisha kwa furaha kwa usemi TGIF(THANKS GOD ITS FRIDAY) wewe tayari umejiweka kwenye kundi la watu ambao hawawezi kufanikiwa kupitia ajira.
Ninachotaka uondoke nacho hapa leo na uanze kukitumia mara moja ni hiki; wewe umejiajiri mwenyewe, na kazi unayofanya ni yako mwenyewe. Jua majukumu yako na kila siku yatimize kwa ufanisi mkubwa, angalia ni hatua gani ya ziada unayoweza kwenda. Kila siku jiulize ni thamani gani unaweza kuongeza kwenye kazi yako. Jitolee kupokea majukumu zaidi na wakati mwingine omba majukumu ambayo unaona hayafanyiwi kazi na yafanyie kazi kwa muda wako wa ziada. Hivi utakuwa umeimiliki kazi unayofanya na hakuna cha kukuzuia kufikia mafanikio.
Lakini utasema siwezi kufanya hivyo, hata hivyo wananilipa mshahara kidogo, sitaki kuonekana nina kiherehere. Na ndio maana mpaka sasa kazi yako inakusumbua. Hivyo chagua kuendelea kufanya unavyofanya sasa na uendelee kupata hiko unachopata, au chagua kufanya nilichokushauri hapo juu na uanze kuona tofauti. Ni rahisi kama hivyo, maisha ni yako na maamuzi ni yako.
SOMA; Tabia Tano(5) Za Wafanyakazi Ambao Ni Sumu Kwenye Eneo La Kazi Na Jinsi Ya Kuepuka Kuwa Mmoja Wao.
Wewe ndiye unayeamua mshahara kiasi gani ulipwe.
Makirita sasa hapa unatudanganya, mimi nimekuwa nafanya kazi kweli lakini mshahara siongezwi, na nimeshalalamika na kuandamana mara nyingi niongezwe mshahara lakini siongezwi. Pole sana kama unapitia hili, lakini jibu rahisi ni kwamba hujafanya hiko nilichoshauri hapo juu. Nenda kaanze kukifanya sasa halafu baada ya muda utaona majibu kwenye mshahara wako, lazima utaongezeka.
Ukweli ni kwamba wafanyakazi wengi wanaamini kwamba kipato wanachopata hakiendani na kazi wanayofanya, yaani ni kidogo sana. Ilikuwa hivyo zamani, ila kwa zama hizi, wengi wanajidanganya. Kikubwa ambacho nimekiona, hasa kwa sekta binafsi, wafanyakazi wengi wanalipwa kidogo kwa sababu hata thamani wanayotoa kwenye kazi zao ni kidogo.
Sikiliza, hakuna mtu ambaye haoni thamani inayozalishwa. Kwa mfano tuseme wewe umeajiriwa kama afisa mauzo, na kwa kufanya kwako kazi kwa kujituma ukaongeza mauzo sana, unafikiri watu hawataona hilo? Unafikiri kuna mtu ambaye hangependa kufanya kazi na wewe? 
Unaamua mshahara wako mwenyewe kutokana na thamani unayotoa kwenye kazi yako. Kama unatoa thamani kubwa, mwajiri wako hatapenda kukupoteza, na wakati huo huo washindani wa mwajiri wako watakuwa wanakuwinda, na hivyo thamani yako kwa malipo inaongezeka sana. Lakini kama unafanya kazi ya kawaida, unasubiri usukumwe, kila siku ugombezwe, mbona hujafanya hiki, mbona hujafanya kile, halafu tena uanze kuwapigia watu kelele kwamba mshahara ni mdogo!! Unapoteza muda na nguvu zako, ni bora uzitumie kuongeza thamani kwenye kazi.
Unalipwa kutokana na thamani unayotoa kwenye kazi yako, kama unacholipwa kwa sasa hakikutoshi, ongeza thamani. Angalia ni jinsi gani unaweza kufanya zaidi, kuongeza ufanisi, na kipato chako kitaongezeka kama utafanya hivyo.
Utaniambia mimi nimeajiriwa serikalini na hivyo hata nikiongeza thamani mshahara haubadiliki sasa, ni mpaka serikali iongeze na inaongeza kwa wote tu. Na mimi nitakwambia fikra hizo ndio zinakufanya huoni kipato kikubwa. Anza kufanya hayo niliyokushauri hapo juu, hata kama upo kwenye ajira ya serikali, na utashangaa kuna fedha nyingi zinakujia nje ya mshahara, tena fedha halali, sio rushwa au hongo.
Nimalize kwa kusema na kusisitiza kwamba, japokuwa upo kwenye ajira, hakuna aliyekuajiri bali ni wewe mwenyewe. Na hata kipato unachopata kinatokana na thamani unayotoa kwenye kazi yako. Anza kufanyia kazi mambo hayo na utaona mabadiliko makubwa kwenye kazi yako na hata mafanikio yako.
Nakutakia kila la kheri kwenye kufanya kazi iliyo bora sana kwako na hivyo kujijengea mafanikio makubwa.
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz