Rais wa Sudan Kusini Asaini Makubaliano ya Amani


Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir, ametia saini makubaliano ya amani Jumatano, kumaliza miezi 20 ya vita ya wenyewe kwa wenyewe, lakini akatoa orodha ya masuala muhimu yanayotia wasiwasi  akionya kwamba mpango huo unaweza usiwe wa muda mrefu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la ufaransa,  AFP,  sherehe za  kutia saini zilifanyika katika mji mkuu Juba, mbele ya viongozi wa kikanda waliofika saa kadhaa baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, kutishia hatua za haraka za vikwazo kama Rais Kiir, atashindwa kusaini makubaliano ambayo tayari yalikuwa yamesainiwa na kiongozi wa waasi Riek Machar.
Katika  hafla hiyo ambayo pia ilihudhuriwa na Wanadiplomasia na Wanahabari,  Rais Kiir, alisema kwamba makubaliano ya amani  ambayo wametia saini yana mambo mengi  ambayo angeweza kuyakataa, na masuala hayo yakipuuzwa  hayatakuwa na maslahi ya nchi  na kuleta amani ya kudumu.
Japokuwa orodha ya masuala yanayomtia wasiwasi iliyogawanywa, makubaliano ya amani yamepongezwa na viongozi wa kikanda ikijumuisha Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, ambaye alituma vikosi vyake kusaidia vikosi vya Rais Kiir, ambapo kwa mujibu wa makubaliano hayo vikosi vina siku 45 kuondoka.
Makubaliano hayo yanaungwa mkono na muungano wa mataifa nane  wanachama wa  IGAD, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Afrika, China,  Uingereza, Norway na Marekani ambazo zimetaka pande zote mbili kumaliza mapigano na kutekeleza  sitisho la kudumu la  mapigano ndani ya saa 72.