Polisi nchini Kenya walisema wamewakamata watu wanane kwa shutuma za jaribio la kujiunga na kundi la wanamgambo la Al-Shabaab la nchini Somalia. Maafisa wa Garissa walisema wanaume hao wanane walikamatwa katika mji wa Dadaab hapo Jumatatu.
Mratibu wa kieneo wa amani na usalama, Mohamud Ali Saleh alisema watu hao wanatokea nchini Tanzania. Hakutoa maelezo zaidi. Bwana Saleh alisema polisi pia wamewakamata wanawake wawili wiki iliyopita katika jimbo la kaskazini-mashariki. Alisema wanawake hao mmoja raia wa Kenya na mwingine raia wa Tanzania walichukuliwa kuandikishwa kama wake katika kundi la Al shabab.
Katika tukio tofauti polisi walivamia nyumba moja ambako walifanikiwa kukamata silaha zikiwemo bastola saba, maguruneti saba ya mkono na risasi 20 na makasha 15 ya kuhifadhia risasi. Bwana Saleh alisema vijana kadhaa walikamatwa kwa kuhusishwa kuwa na silaha lakini hakueleza idadi ya washukiwa hao.
Bwana Saleh aliwasihi wakazi kuwa waangalifu kwa watu wanaotafuta nyumba kwa ajili ya kupanga.
Mji wa Garissa umekuwa ukilengwa na mashambulizi ya Al-Shabaab. Hapo April mbili mwaka 2015 kundi moja la Al-Shabaab lilishambulia chuo kikuu cha Garissa na kusababisha vifo vya watu 148 wengi wao wakiwa wanafunzi