Mahakama Burundi yaidhinisha ushindi wa Nkurunziza


Mahakama ya katiba ya Burundi imeidhinisha ushindi wa Pierre Nkurunziza katika uchaguzi wa Rais wa hivi karibuni nchini. 

Mahakama ya katiba ya Burundi imetangaza kuwa hakuna uvunjaji wa kanuni ulioshuhudiwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika hivi karibuni nchini humo. 

Mahakama hiyo pia imesema kura za uchaguzi wa Rais wa Burundi zimehesabiwa kwa mujibu wa sheria na hakuna mgombea yoyote wa kiti cha urais aliyewasilisha ombi la kutaka kuhesabiwa upya kura hizo. 

Hii ni katika hali ambayo Jumatatu iliyopita Abubakar Zein mwenyekiti wa ujumbe wa wasimamizi wa uchaguzi kutoka Jumuiya ya Afrika Mashariki yaani taasisi ya kieneo inayoundwa na Burundi, Uganda, Tanzania, Kenya na Rwanda aliutaja mchakato wa uchaguzi wa Burundi kuwa uliokuwa na kasoro kutokana na kutokuwepo usalama, kujiri mivutano mikali, kubanwa vyombo vya habari, kukiukwa haki za msingi za binadamu na uhuru wa kiraia na kisiasa. 

Kwa mujibu wa matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza amepata asilimia 70 ya kura zilizopigwa.