WAKUNGA Mkoani Njombe
wamefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama wakati wa kujifungua mwaka jana
kutoka 27 mwaka juzi na kufikia 21 ambapo zaidi ya wanawake 23,000 walifika
kituoni kujifungua.
Akizungumza katika
maadhimisho ya siku ya wakunga Mkoani hapa kitaifa, mratibu wa mzazi na mtoto
mkoa wa Njombe Felisia Hyera, alisema kuwa kati ya wanawake 23,736
waliojifungua mwaka 2014 akina mama 21 walifariki kutokana na matatizo wakati
wa kujifungua.
Alisema vifo hivyo
vimepungua kutoka 27 mwaka 2013 kati ya akina mama 20,149 walio fika
hospitalini kujifungua na kuwa kiwango kiliongezaka mwaka jana na vifo
vilipungua.
Alisema kuwa vifo hivyo
vimepungua kutokana na kuwapo kwa utendaji thabiti wa wakunga katika hospitali
za mkoa huo.
Hyera aliongeza kuwa
kiwango cha waja wazito kujifungulia katika vituo vya afya kimeongezeka kwa
asilimia 94 mwaka jana huku mwaka juzi ilikuwa ni asilimia 90.
Alisema kuwa mafanikio
hayo yamekuja ni kwa nguvu za ushirikiano baina ya serikali, mashirika ya dini
na wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake mkuu wa
wilaya ya Njombe Sarah Dumba alisema kuwa kwa miaka ya nyuma kulikuwa na gumzo
kwa akina mama wakienda hospitali hasa hospitali ya Kibena kuwa wakifika huko
watakufa.
Alisema kuwa watu
walikuwa na wasiwasi wa wake au ndugu zao kufa wakifikishwa katika hospitali
hiyo lakini kwa sasa vifo vimepungua ambapo vikitokea vina tokea kwa bahati
mbaya.
Alisema kuwa
halmashauri zinawajabu wa kuomba serikali kuwaletea madaktari wakunga katika
hospitali zao ambapo katika hospitali ya Kibena kuna Daktari mkunga mmoja
pekee.
“Halmashauri mna wajibu
wa kuomba serikali kusajili Daktari mkunga katika hospitali za halmashauri ili
kuboresha zaidi watu wanao leta kizazi cha baadae kama kauli mbiu yenu
inavyosema,” alisema Dumba.