Wakazi wa Kijiji cha Lugenge wamesusa kuuzika mwili wa
Marehemu Basili Mwalongo (24) mkazi wa Mtaa wa Kambarage Mjini Njombe aliyeuawa
na askari polisi wa doria siku ya Jumanne wiki hii.
Marehemu Mwalongo alikuwa azikwe mjimbani kwao katika kijiji
na kata ya Lugenge jana, lakini ilishindikana kwa kile kinachodaiwa kuwa
kutokana na serikali kushindwa kutoa kibali cha kifo cha marehemu
kinachozingatia taratibu zote za kisheria badala yake ilitoa kibali kisicho
kuwa na sahihi wala mhuri wa kiongozi yoyote wa serikali.
Aidha kibali hicho ambacho Elimtaa nakala lilikiona
hakina maelezo ya Daktari kuhusu sababu zilizopelekea kifo cha mtu huyo.
Akizungumza na Elimtaa msemaji wa familia, Joseph
Mwalongo, alisema wamegoma kuuzika mwili huo kufuatia dosari zilizojitokeza
katika kibali hicho, na kwamba kama serikali kupitia ofisi ya mkuu wa mkoa
haitarekebisha kibali hicho watairudisha maiti kituo cha polisi ili wazike
wenyewe wanavyojua.
“Sisi kama ndugu tulitafuta sababu za kuawa ndugu yetu
hatukupata sababu, tumepata karatasi ya kibali haina mhuri wala sahihi yoyote
tukaamua kwenda kwa mkuu wa wilaya ya Njombe ili kutafuta haki,” alisema
Mwalongo na kuongeza.
“Nashangaa hata Mkuu wa Kituo cha Polisi Njombe hakutuma
mwakilishi katika mazishi haya wakati waliotekeleza mauaji haya ni polisi sasa
tunajiuliza haki iko wapi? Alihoji.
Shuhuda wa tukio hilo Rose Mayemba, alisema wananchi
walifikia maamuzi ya kususia mazishi hayo kutokana na polisi kushindwa kutuma
uwakilishi kama walivyoafikiana jana katika kikao cha ulinzi na usalama jana,
na pia hawakujua baada ya mazishi nini kutatokea kutona na kibali kilichotolewa
kutokuwa na mhuri na sahihi za viongozi
hali iliyozua sintofahamu hadi kupelekea kuundwa tume ya watu nane kwenda Mkuu
wa Wilya ya Njombe Sarah Dumba ili kujua hatua ya jambo hilo.
“Wananchi wamegoma kabisa kuzika kwa sababu kibali
walichopokea hakina mhuri wala sahihi sasa wanahofu wakizika watajuaje huyu mtu
amekufa kwa sababu gani,” alisema Mayemba.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe Franco Kibona jana
alipofuatwa na waandishi wa habari kutolea ufafanuzi tukio hilo alisema hawezi
kulizungumzia kwa kuwa alikuwa hajakamilisha taarifa zote na kuahidi kulitolea
ufafanuzi leo ya saa sita mchana.
Hatua inakuja kufuatia siku ya Jumanne majira ya saa 3 usiku
polisi wa doria kudaiwa kumuua mtu huyo eneoa Zengelendete Mtaa wa Kambarage na
kumjeruhi mwingine Fred Sanga aliyelazwa katika Hospitali ya Kibena kwa
matibabu walipokuwa wanakunywa pombe katika klabu cha Nyondo.
Hali hiyo ilisababisha juzi wakazi wa Njombe kuandama
wakipinga mauaji hayo ya polisi dhidi ya raia na kuwalazimu polisi kutumia muda
wa zaidi ya saa tano kuwatawanya kwa mabomu ya machozi.