Marseille v PSG; Arsenal v Liverpool

“Katika historia ya Ligi Kuu ya England mechi kati ya Arsenal na Liverpool ndizo zinaongoza kwa kuwa na ‘hat trick’ nyingi zikifungwa  tano.”

Ligi Kuu ya England (EPL) inarudi tena viwanjani ikiungana na ligi nyingine barani Ulaya baada ya majukumu ya kitaifa kukishuhudiwa mechi za kufuzu za UEFA Euro 2016 na mechi za kirafiki za kimataifa.

Kabla hatujasonga mbele katika kuimulika EPL katika mchakamchaka wa wikiendi hii, tujikite katika mechi tatu kali nje ya ligi ya England

Marseille v Paris Saint Germain
Paris Saint Germain (PSG) ipo kileleni mwa ligi kuu nchini Ufaransa kwa alama 59 ikifuatiwa na Lyon alama 58 huku nafasi ya tatu ikishikwa na Olympique de Marseille yenye alama 57.
Desemba 1971 walikutana kwa mara ya kwanza na Josip Skoblar alifunga mawili wakishinda 4-2 dhidi ya PSG. 

Wamekutana mara 85, PSG ikishinda mara 33, Marseille mara 32 na wakitoka sare mara 20.
Endapo PSG itashinda utakuwa ni ushindi wa saba mfululizo dhidi ya Marseille katika michuano yote. Mwaka 2002 na 2004 PSG iliweka rekodi ya kushinda michezo nane ikienda kuwakabili wakali hawa wa Provence-Alpes-Côte d'Azur

Aidha Kocha Laurent Blanc amekuwa na matokeo mazuri dhidi ya Marseille tangu alipoteuliwa kuinoa PSG mwaka 2013.

Wachezaji Claude Makelele, Gabriel Heinze na George Weah wamecheza vilabu hivi kwa nyakati tofauti.

Dortmund v Bayern Munich
Mshambuliaji wa Bavarians Robert Lewandowski anatarajiwa kurudi kwa mara nyingine tena katika klabu yake ya zamani kwenye mtanange wa kihasimu “Der Klassiker”

Mkali huyo wa Poland aliyefunga mabao 13 katika mitanange 24 ya ligi msimu huu alisema ataendelea kutunda uhusiano mzuri na BVB kwani alipata mafanikio makubwa katika miaka minne aliyoitumikia klabu hiyo.

Bayern wanajipanga kwa ajili ya kulitwaa kombe la Bundesliga kwa mara ya tatu mfululizo wakiwaacha VfL Wolfsburg kwa pointi 10.

Itakumbukwa kwamba misimu miwili iliyopita BVB 09 ilimaliza ya pili katika ligi hiyo ndoto ambayo msimu huu imepotea kabisa.

Dortmund ipo nafasi ya 10 ikijinasua kutoka mkiani; haijapoteza mchezo hata mmoja katika mechi saba mfululizo.

Bavarians walipunguzwa kasi na Borussia Monchengladbach kwa mabao 2-0.
Aidha Bayern itakosa huduma  David Alaba, Arjen Robben, Javier Martinez, Frank Ribery na Thiago Alcantara.

Tegemeo kubwa la Dortmund limebebwa na raia wa Gabon Pierre Emerick Aubameyang alitupia mawili dhidi ya Hannover waliposhinda mabao 3-2.

Celta Vigo v Barcelona
Kocha Luis Enrique anarudi kwa mara nyingine katika uwanja wa Balaidos kabla ya kutimkia Barcelona alikuwa akiinoa Celta de Vigo.

Novemba mwaka uliopita Barca walipoteza mchezo dhidi ya Celta de Vigo wakinyukwa 1-0 na kuweka rekodi ya kwanza kushinda Nou Camp wakifanya hivyo mara ya mwisho mwaka 1940.

Barcelona inatarajiwa kuendelea kuitumia safu ya MSN-Messi, Suarez na Neymar katika safu ya ushambuliaji.

Baada ya kuangazia kurunzi letu katika ligi tatu tofauti barani Ulaya , turudi katika viwanja mbalimbali nchini Uingereza.

Arsenal v Liverpool
Kocha Arsenal Wenger amejinasibu kuwa kikosi chake kipo sawa kuwavaa majogoo wa Liverpool watakapotua Kaskazini mwa London.

Arsenal imeshinda mechi 9 katika 10 ilizocheza katika EPL huku kocha huyo akifuta mawazo ya kutwaa ubingwa kutokana na kuachwa alama saba na Chelsea waliopo kileleni.

Liverpool ilipoteza mchezo wake dhidi ya Manchester United ilipokubali mabao 2-1 Merseyside na kufuta rekodi ya kutofungwa tangu mwaka 2015 uanze katika EPL.

Brendan Rodgers ana matumaini makubwa ya kumtumia Daniel Sturridge na Adam Lallana huku Raheem Sterling akiwa njiapanda.

Liverpool itakosa huduma ya mlinzi wa kati Martin Skrtel na Steven Gerrard kwani wanaendelea kutumikia adhabu.

Arsenal itamkaribisha Jack Wilshere na Danny Welbeck huku Alex Oxlade-Chamberlain akiwa njiapanda

Mikel Arteta, Mathieu Debuchy na Abou Diaby waliocheza mechi ya kirafiki dhidi ya Brentford juma hili bado haijathibitishwa kama watakuwemo au la.

Itakumbukwa kwamba katika historia ya Ligi Kuu England mechi kati ya Arsenal na Liverpool ndizo zinaongoza kwa kuwa na ‘hat trick’ nyingi zikipatikana  tano.