FC Platinum mdomoni mwa Yanga SC




Kikosi cha FC Platinum, Machi 2015
Klabu ya Yanga ipo njiani kuelekea nchini Zimbabwe kuikabili FC Platinum inayoshiriki Ligi Kuu nchini humo, ikiwa ni mzunguko wa pili wa Kombe la Shirikisho barani Afrika.


Mechi hiyo itachezwa wikiendi hii, ambako wenyeji FC Platinum licha ya matumaini yao ya kusonga mbele kufifia baada ya kichapo cha mabao 5-1 walipotua jijini Dar es Salaam lakini watahitaji kuwaonyesha mashabiki wao kuwa bado wanaweza.

Zimbabwe ni miongoni mwa nchi, hapa barani Afrika yenye kiwango bora cha soka. 

Itakumbukwa kwamba Yanga ikifaulu mtihani dhidi ya wabishi hawa wa Zvishavane itakumbana na kitimutimu kutoka Angola au Tunisia.
Kikosi cha Yanga, Machi 2015

Leo tuangazie FC Platinum na mwenendo mzima kuelekea mtanange huu dhidi ya Yanga SC.

FC Platinum
Klabu ya soka ya FC Platinum ilianzishwa mwaka 1995 ikijulikana kwa jina la Mimosa FC ambapo mwaka 2010 waliibadilisha na kuiita FC Platinum. 

Ina maskani yake katika wilaya ya Zvishavane, Jimbo la Midlands nchini Zimbabwe. Mwenyekiti wa klabu hiyo kwa sasa ni Dumisani Sisale. Inatumia uwanja wake wa Mandava wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 15,000.

Jimbo la Midlands lenye makao makuu katika mji wa tatu kwa ukubwa wa Gweru lipo katikati ya Zimbabwe.

Mtanange wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Yanga utachezeshwa na waamuzi kutoka Angola, Helder Martins de Carvalho, Jerson Emiliano dos Santos and Wilson Valdmiro Ntyamba katika uwanja wa Mandava. 

Ligi kuu nchini humo imeshaanza “Castle lager Premiership” kukishuhidwa mwanzo mbaya wa FC Platinum ilipokubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Caps United jijini Harare.

Kocha wa FC Platinum Norman Mapeza hakuonekana kushtuka kwa kipigo hicho akizungumza kwa kujiamini alisema “Ni mapema mno kusema kwamba nimeshindwa, hata hivyo kupoteza mchezo hutokea katika soka, tunaendelea kufanya kazi na matokeo yatakuja” 

Klabu hiyo ina wachezaji wazuri akiwemo Walter Musona ambaye katika mechi ya ufunguzi katika ligi hiyo alionekana kufanya kazi nzuri upande wa kushoto akitumbukiza mipira ndani lakini ilikuwa ikiishia kwa walinzi wa timu pinzani.

Pia Musona alikuwa hatari kwa mipira ya vichwa hususani katika dakika ya 70 alipopokea mpira uliotumbukizwa ndani na Mutasa alipoupiga na kutoka nje kidogo ya lango.

Waliocheza katika mechi hiyo wanaojitayarisha kuivaa Yanga walikuwa Petros Mhari, Gift Bello, Ian Nekati, Kelvin Moyo, Aaron Katebe, Thabani Kamusoko, Wisdom Mutasa (Allen Gahadzikwa, 66′), Simon Shoko (Wellington Kamudyariwa, 57′), Walter Musona, Donald Ngoma (Obrey Chirwa, 80′), Brian Muzondiwa.

Itakumbukwa kwamba FC Platinum haijashinda mchezo hata mmoja kati ya mitatu iliyopita, ikizabuliwa na Yanga 5-1 katika mzunguko wa kwanza wa Kombe la Shirikisho, imetoa sare ya 2-2 dhidi ya timu iliyopanda daraja msimu huu ya Dongo Sawmills kisha  imepigwa na Caps United bao 1-0.

Wachezaji wa kuchungwa
Donald Ngoma ni miongoni mwa washambuliaji wazuri katika ligi kuu nchini humo, itakumbukwa kwamba akitoka majeruhi aliisawazishia FC Platinum dhidi ya Dongo Sawmills.

Pia Musona ni mchezaji tegemeo anayejituma sana, ana uwezo mkubwa wa kutupa mipira mirefu, kuitumbukiza ndani ya eneo la hatari na inapotokea mkwaju wa penati ni hatari.

Aliisawazishia FC Platinum kwa mkwaju wa penati katika dakika 24 kabla ya Dongo Sawmills kuongoza.

Kelvin Moyo, Wisdom Mutasa na Walter Musona wapo katika kikosi cha Timu ya Taifa “Young Warriors” chini ya umri wa miaka 23 
 
Je wajua?
Mji wa Zvishavane hapo awali ulikuwa ukijulikana kwa jina la Shabani hadi mwaka 1983. Zvishavane linatokana na neno la watu wa kabila la Shona, likiwa na maana ya “Red Hills”.

Zvishavane ni mji uliozungukwa na miinuko ya hapa na pale ukiwa na wakazi wapatao 45,230 (kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012) walio wengi wakijishughulisha na uchimbaji wa madini.

FC Platinum ilitwaa tuzo ya timu yenye nidhamu msimu mwaka 2014 nchini Zimbabwe. Imeshiriki Ligi ya Mabingwa mara moja tu hii ilikuwa mwaka 2012/2013

Hii ni mara ya kwanza kushiriki Kombe la Shirikisho.

kwa hisani ya Jaizmelaleo