AIBU ya mwaka! Mwanadada aliyefahamika kwa jina la Tatu Ally (26), mkazi wa Kongowe, Mbagala, Dar amejikuta akiifedhehesha familia yake kufuatia kutoroka kwa mumewe siku moja tu baada ta kufunga ndoa, Amani lina picha kamili.
Mwanadada Tatu Ally anayedaiwa kutoroka baada ya kufunga ndoa.
Kwa mujibu wa chanzo, ndoa hiyo ilifungwa Aprili 4, mwaka huu Mbagala jijini Dar kisha bi harusi huyo kwenda kwa mumewe aliyetajwa kwa jina moja la Ramadhani kule Mbezi ya Kimara, Dar ambapo Aprili 5 aliingia mitini.
Chanzo kikadai kwamba, bibi harusi huyo aliamua kuchukua uamuzi huo kwa sababu alikuwa na mwanaume mwingine ambaye angefunga naye ndoa.
Chanzo cha kuaminika kinaeleza kwa kina kuwa mwanadada huyo alishaolewa na mwanaume mwingine akatoroka na amekuwa na tabia za ajabuajabu kiasi kwamba watu wanamchukulia kama anafanya biashara ya kujiuza.
KISIKIE CHANZO
“Kusema kweli alichofanya dada Tatu ni kibaya sana, siwezi kusema sana lakini tukio hilo limemuuma kila mtu hapa mtaani.“Baada ya tukio la kutoroka, sasa mumewe anataka arudishiwe mahari yake (haikutajwa ni kiasi gani) sambamba na gharama zote zilizotumika siku hiyo ikiwemo usafiri na chakula kitu ambacho hakiwezekani.
“Familia imekaa kikao na kujadili juu ya tukio hilo lakini Tatu mwenyewe yupo mitaa ya Toangoma njia ya kwenda Kigamboni (Dar), tunasikia anataka kuolewa tena Jumanne (juzi),” kilisema chanzo.
Bwana Ramadhani anayedaiwa kutorokwa na mkewe baada ya ndoa.
BABA MZAZI ATOA NENO ZITO
Naye baba mzazi wa Tatu, mzee Ally alipotafutwa na Gazeti la Amani juzi ili azungumzie tukio hilo la binti yake kutoroka kwa mume siku moja baada ya ndoa, alikuja juu na kusema kuwa hataki kumuona (Tatu) wala kumsikia kwa lolote kutokana na aibu waliyoipata kama familia.
“Sitaki hata kumsikia masikioni mwangu na kwanza si mwanangu tena nimemtoa hata kwenye orodha ya watoto wangu. Yeye hakulazimishwa kuolewa alitaka mwenyewe na nikamuuliza kama anataka sherehe akakataa na kudai kuwa anataka dua tu na ndiyo tukafanya hivyo kama alivyotaka lakini yeye ametupa aibu kubwa sana hapa mtaani.
“Mtoto hatulii sijui amekuwaje jamani? Sasa nasema hivi kwa aibu aliyonipa sitaki kumuona tena na kama anaolewa basi ajiozeshe mwenyewe huko aliko mimi nimechoka kabisa siwezi na ulimi wangu hauwezi kuziba pua yangu.
“Hatujui aliko mpaka leo hii na hapatikani kabisa hata kwenye simu yake ya mkononi tunasikia ana namba za simu nyingi ila tumeshakwenda kutoa taarifa polisi kwa upande wetu sisi wanafamilia na kwa upande wa mume wake naye nilimshauri akatoe taarifa polisi huko kwao Mbezi,” alisema kwa jazba baba wa Tatu.
MUME HATAKI MASWALI
Akizungumza kwa njia ya simu na Amani huku sauti yake ikiwekwa kwenye kifaa cha kumbukumbu, mwanaume aliyemuoa Tatu ambaye anadaiwa kutaka arejeshewe mahari yake alisema:
“Sihitaji kuulizwa kitu chochote, naomba mniachie mwenyewe nifuatilie suala hili mpaka mwisho.”
Ramadhani na mkewe siku ya ndoa yao.
BI HARUSI MWENYEWE SASA
Tatu alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi naye akarekodiwa, alijitetea na kudai kuwa yupo mkoani Morogoro na aliamua kuondoka kwa mume wake kwa sababu ya matatizo aliyokutana nayo huko na kukanusha taarifa za kutaka kuolewa upya.
“Niko Morogoro sasa hivi, sijatoroka niliamua kuondoka kwa yule bwana aliyenioa kwa sababu kuna matatizo yalinikuta ndiyo nikaona niondoke na aliyewaambia kuwa nataka kuolewa tena ni muongo, mimi siwezi kujiozesha mwenyewe.
“Kwanza (wazazi) wamekwambia wamenipa shilingi ngapi? Wao wanataka watajirike kupitia mimi, yaani katika mahari yote eti mimi wanipe shilingi laki mbili tu na wao wachukue laki sita wapi na wapi!” alisema Tatu.
Kwa madai hayo ya Tatu, mahari ya kuolewa kwake ilikuwa shilingi laki nane (800,000).
Hata hivyo, Jumanne iliyopita gazeti hili lilifuatilia kwa karibu ili kujua kama Tatu atafunga ndoa tena au la! Mpaka gazeti linakwenda mitamboni, chanzo kilisema Tatu alionekana mitaa ya Kigamboni mchana wa siku hiyo akifanya ‘window shopping’