Ndoa ya Lulu Michael Mwaka 2014 Yabuma, Mwenyewe Asema Hajilaumu Mungu Ndo Kapanga

BAADA ya kuwa na malengo ya kuolewa mwaka 2014, mwigizaji Elizabeth Michael ‘Lulu’ ameibuka na kusema imeshindikana lakini hajilaumu wala hamlaumu mtu yeyote kwa kutotimiza suala hilo kwani anaamini Mungu ndiye anayewezesha kila kitu.

Akizungumza na paparazi wetu hivi karibuni, Lulu alisema mwaka 2014 alikuwa na malengo mengi likiwemo suala la ndoa lakini kwa kuwa Mungu ndiye muweza, atapanga upya suala hilo na anaamini litakuja kutimia.

“Ndoa ni mipango ya Mungu, huwezi kulazimisha hata siku moja, sisi wanadamu huwa tuna mipango yetu lakini ili ifanikiwe lazima kuwe na baraka za Mungu,” alisema Lulu. 
Akizidi kupiga stori na paparazi wetu, Lulu alisema kwa mwaka huu na mwakani hawezi kuweka malengo ya ndoa kwani bado kuna mambo yake hajayaweka sawa hivyo suala la kuolewa ataliweka hadharani baada ya miaka miwili ijayo.

“Sina mpango hata kidogo kwa mwaka huu wala mwakani labda baada ya hii miaka kupita ndiyo ninaweza kupanga tena suala la ndoa,” alisema Lulu.
Alipotakiwa kumtaja mpenzi aliyenaye kwa sasa, Lulu aligoma kufunguka lakini akakubali kuanika siri za mwanaume anayetaka kuwa mumewe.

“Kwanza nahitaji mwanaume atakayenielewa kwa kila kitu, pia awe na mapenzi ya kweli na atakayeniangalia kama Lulu na siyo kama Elizabeth pekee. Anapaswa kutambua na kusapoti kazi zangu za sanaa,” alisema Lulu.

Kuhusu mikakati yake ya sanaa mwaka huu, Lulu alisema ana mpango wa kuendelea na masomo huku akiwa pia na ‘project’ kubwa mbili ambazo anatarajia kuzifanya.
“Nina project kubwa mbili mwaka huu, muda utakapofika kila mmoja atazijua maana nitaziweka wazi,” alisema Lulu