Kundi la Boko Haram limedai kuwa wasichana wa shule 219 waliotekwa nyara
zaidi ya miezi sita iliyopita wamebadili dini kuwa waislamu na wameolewa.
Hatua hiyo imezishangaza familia za wasichana hao na kuthibitisha uvumi
kuhusu madai ya kuwepo makubaliano ya kuwaachia huru na kuwataka
wanamgambo hao wasitishe mapigano. Kiongozi wa Boko Haram, Abubakar
Shekau, ameyasema hayo katika mkanda wa video ambapo pia amekanusha
madai ya serikali ya kuwepo mkataba wa kumaliza uasi na kuanzisha
mazungumzo ya amani. Shekau pia amedai kuwa kundi hilo lilihusika na
utekaji nyara wa raia wa Ujerumani, aliyekamatwa kutoka nyumbani kwake
katika jimbo la kaskazini mashariki, Adamawa mnamo Julai 16.