Ngome za IS zashambuliwa Syria

Ngome za wapiganaji wa kundi linalojiita "Dola la Kiislamu", IS, nchini Syria karibu na mpaka wa Uturuki zimeendelea kushambuliwa jana usiku. Kwa mujibu wa Rami AbdulRahman kutoka kundi la haki za binaadamu linalofuatilia matukio nchini Syria, ndege za kivita zilizofanya mashambulizi hayo magharibi mwa mji wa Kobani unaojulikana pia kama Ayn al-Arab, zilitokea upande wa Uturuki. Hata hivyo, Waziri wa Mkuu wa Uturuki, Ahmet Davutoglu, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba si anga la nchi yake wala kituo cha kijeshi cha Marekani kwenye ardhi yake kilichotumika kwenye mashambulizi hayo. Muungano unaoongozwa na Marekani ulianza kufanya mashambulizi ya angani dhidi ya kundi hilo la IS ndani ya Syria usiku wa kuamkia jana.
Wiki iliyopita, kundi hilo la itikadi kali lilifanya mashambulizi dhidi ya mji huo wa Kobani wenye wakaazi wengi wa Kikurdi na kusababisha Wakurdi wa Kisyria zaidi ya 130,000 kukimbilia Uturuki.