Askofu Cheyo wa Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, akanusha waraka

Askofu Alinikisa Cheyo wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi lililo na Makao yake Makuu eneo la Jacaranda Jijini Mbeya amekanusha waraka unaosambazwa ili kumshinikiza ajiuzuru nafasi ya Uaskofu.
Cheyo (Pichani) amesema waraka unaodaiwa kusambazwa na Baraza la Wazee wa Ushirika wa Bethelehem bado hajaupata ofisini kwake na kwamba kitendo hicho ni kukiuka maadili ya utumishi wa Kanisa na Katiba ya Moravian Jimbo la Kusini Magharibi.
Waraka huo uliosambazwa katika Shirika mbalimbali na Taasisi za Kanisa na kufanikiwa kupata nakala yake ukiwa umesainiwa na Katibu wa Baraza R. Kalinga na Mwenyekiti wa Baraza Mchungaji wa Ushirika wa Bethelehem Edward Chilale.
Askofu Cheyo ambaye yuko kikazi Dodoma alisema kuwa kitendo kilichofanywa na Mchungaji Chilale ni cha utovu wa nidhamu na anafanya hivyo kujihami kutokana na maamuzi magumu na  hatua ambazo zinatarajiwa kuchukuliwa na Halmashauri Kuu ya Jimbo.

 Hata hivyo Wachungaji wengine walisema hawakubaliani na waraka uliotolewana Baraza la Bathelehem na kwamba hizo ni chuki binafsi za Mchungaji Chilale baada ya kuonywa kuacha biashara za Pentagon,Elimisha na Madawa ya GNLD ambapo amekuwa akikusanya fedha kutoka kwa waumini na wasio waumini.
Wachungaji hao ambao hawakupenda kutaja majina yao walisema pia Mtunza hazina wa Ushirika huo ambaye pia ni Mtumishi wa Umma ndiye amekuwa akiufadhili mgogoro huo kwa kutoa gari lake na kusambaza barua za uchochezi katika shirika mbalimbali.
Wameenda mbali zaidi kwa kusema kuwa kama ni maamuzi ya Baraza la Bethelehem iweje waraka huo usambazwe katika sharika nyingine wakati kila baraza lina maamuzi yake hivyo ni kuingilia utaratibu na kuwanyima waumini na Taasisi uhuru wa kujadili agenda zao.
Mgogoro huo umekuwa ukizidi kushika kasi siku za hivi karibuni na kuzidi kuligawa Kanisa kimwili na kiroho kwani badala ya kujadili maendeleo ya Kanisa, waumini na Viongozi wamekuwa wakipoteza muda kujadili mgogoro bila kupata ufumbuzi wowote

Na Mbeya Yetu Blog