Jeshi la Syria limepiga hatua kuelekea katika maeneo yanayoshikiliwa na makundi ya Kiislamu katika kijiji cha kaskazini cha Tal Hassel, wakati waasi wa makundi ya Jihad karibu na Aleppo wakitoa wito wa kupata wapiganaji zaidi ili kuzuwia hatua hiyo.
Mapigano yameendelea katika kijiji cha Tal Hassel, kilichoko kilometa 12 kutoka Aleppo, mji wa kale wa kibiashara nchini humo.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la SANA, katika maeneo mengine nchini humo mapigano yameendelea na watu tisa wameuwawa kwa makombora katika mji wa kati wa Homs.
Afisa wa jeshi amethibitisha kuwa jeshi hilo linaelekea katika kijiji cha Tal Hassel, na kuongeza kuwa jeshi linatanua operesheni kuyachukua tena majimbo yanayodhibitiwa na waasi.
