WANANCHI WAWAVAMIA MAAFISA MAZINGIRA, MOJA WAMJERUHI KWA MAPANGA







MLIMA MBEYA
ZAIDI ya maofisa 20 wa idara za misitu kutoka katika halmashauri za Jiji na Mbeya vijijini, wamenusurika kuuawa wananchi wakiwa katika zoezi la kuwaondoa wavamizi katika hifadhi ya msitu wa Mbeya, huku mtu mmoja anayedaiwa kuwaongoza maofisa hao kujeruhiwa vibaya kwa kukatwa na mapanga kichwani.

Mtu huyo aliyejeruhiwa, Yohana Mdewa (54) inadaiwa alikumbwa na mkasa huo kutokana na kudaiwa kuwa kihelele kwa kuwaongoza maofisa hao wa halmashari kwenda kuwaondoa wananchi hao kwa kufyeka mazao yao mashambani.


Tukio hilo lilitokea juzi katika kijiji cha Isengo, kata ya Iziwa, wilayani Mbeya vijijini, ambapo kundi la wananchi wapatao 400 kujikusanya na kuwavamia maofisa hao waliokuwa wakiendesha zoezi la kuwaondoa wananchi hao.


Inadaiwa kuwa zoezi hilo halali la serikali la kuwaondoa wananchi hao lilianza Januari 24 mwaka huu baada ya maofisa zaidi ya 20 kutoka katika halmashauri ya wilaya ya Mbeya na halmashauri ya Jiji, wakiwa na mgambo kuvamia kijiji hicho na kuanza kufyeka mazao.


Habari zaidi zinadai kuwa baada zoezi hilo kufanyika, juzi maofisa hao walirudi tena kwa lengo la kuendelea na oparesheni hiyo, lakini ghafla walijikuta wakivamiwa na kundi la wananchi na kuanza kushambuliwa kabla ya kukimbia na kwenda kujifungia kwenye ofisi za kijiji.

Taarifa hizo zinadai kuwa salama ya viongozi hao ilitokana na jeshi la polisi kupata taarifa mapema na kupeleka askari polisi 20 wakiwa na silaha za moto hali iliyoimarisha ulinzi katika ofisi hizo kabla ya kuwaondoa.
Hata hivyo inadaiwa kuwa wakati polisi wakiwaokoa maofisa hao, baadhi ya wananchi walirudi na kwenda kumalizia hasira zao kwa kuyaharibu magari yaliyokuwa yamewabeba na kuwadfikisha kijijini hapo maofisa hao wa halmashauri hizo na mgambo.

Kamanda wa polisi mkoani hapa, Diwani Athumani, alipohojiwa juu ya tukio hilo alikiri kutokea, huku akisita kueleza kama kuna watu wamekamatwa kwa kuwa jeshi hilo linaendelea na uchunguzi wa kuwabaini vinara wa mpango huo.


Alisema katika tukio hilo, ofisa mmoja kuoka asasi ya kiraia ya utunzaji wa mazingira alijeruhiwa na mali ambazo ni magari ya serikali yaliharibiwa vibaya na wananchi katika vurugu hizo zilizodumu kwa zaidi ya saa mbili kabla ya jeshi hilo kufanikiwa kudhibiti.

Aliyataja magari yaliyoharibiwa kwenye vurugu hizo kuwa ni STJ 1830 mali ya wakala wa hifadhi ya misitu nyanda za juu kusini, ambalo lilipasuliwa kioo cha mbele,pamoja na   kwa STJ 1821 na STJ 1832.


Aidha, Diwani alisema katika kile kinachoonekana kuwa wananchi hao walikuwa wamejipanga kwa ajili ya vitendo hivyo vya uhalifu, walitumia mbinu kali ya kubomoa madaraja mawili katika barabara inayoingia kijijini hapo, baada ya msafara wa viongozi wa oparesheni kupita kwa lengo la kuwadhibiti pindi mapambano yatakapoanza.


Kutokana na hali hiyo, kamati ya ulinzi ya wilaya hiyo ililazimika kukutana ghafla kwa lengo la kuzungumzia mustakhabali wa tukio hilo, ambapo walifikia maamuzi ya kuwa zoezi hilo lazima liendelee kwa ajili ya kudhibiti uharibifu wa vyanzo vya maji.



Hifadhi za msitu wa safu za mlima Mbeya (Mbeya range forest reserve),zilitangazwa lasimi kuwa hifadhi ya akiba katika gazeti la selikali mwaka 1957, ambapo kwa muda wote huo limekuwa likitumika kama chanzo kikubwa cha vyanzo vya maji katika halmashauri hizo mbili za Mbeya Jiji na Vijijini.

Kwa mujibu wa taarifa za pia  wakala wa hifadhi ya misitu nyanda za juu kusini, hifadhi hiyo ya msitu ulikuwa na vyanzo vya maji vya kuaminika 40, lakini kutokana na uvamizi uliofanywa kwa muda mrefu na wananchi, kumebaki na vyanzo 18 tu.

Mwisho.