LOWASA: UZALENDO MUHIMU



NA KALULUNGA BLOG
WABUNGE wa Kamati ya  Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU) na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Dk Asha- Rose Migiro wamesema kuwa Watanzania wanakwenda ndivyo sivyo katika suala la kuthamini uzalendo na kuweka mbele maslahi ya taifa.

Migiro na wabunge hao walitoa kauli hiyo hivi karibuni walipokutana jijini New York, Marekani wakati kamati hiyo inayoongozwa na Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa  ilipofanya ziara kutembelea ofisi za balozi za Tanzania nchi mbalimbali.

Katika mazungumzo hayo kamati hiyo na Dk Migiro walionyesha wasiwasi wao kuhusu suala hilo wakieleza kuwa suala la utaifa na uzalendo, dhana ya  Watanzania kuthamini uzalendo na kuweka mbele maslahi ya utaifa bila ya kujali itikadi zao za kisiasa linalekea kubaya.

Walisema kuwa licha ya Watanzania kuwa na misingi yote inayosisitiza haja na umuhimu wa kuweka maslahi ya utaifa na uzalendo mbele, dhana hiyo imeanza kumong’onyoka, hali inayotishia mustakabali wa taifa.

Katika mkutano huo Lowassa alimpongeza migiro kwa kumaliza jukumu lake kama Naibu Katibu mkuu wa UN akisema: “ Kwa niaba ya wajumbe wa Kamati yangu, tukupongeze kwa kumaliza salama jukumu zito na kubwa, kwa hakika umetuwakilisha na umeipeperusha vema  Bendera ya Tanzania na umeliwakilisha vema Bara la Afrika na  waafrika.”

Alisema kuwa matarajio ya kamati yake ni kwamba Dk Migiro ataendeleza ushirikiano aliokuwa akiutoa kwa kamati yake alipokuwa Naibu Katibu Mkuu atauendeleza  kwa maslahi ya taifa baada ya kurejea nyumbani.

Naye Dk Migiro alisema kuwa atakuwa tayari daima kutoa mchango wake atakapohitajika kwa maslahi ya taifa.

Aliwataka wajumbe wa kamati hiyo, kujijengea uwezo na ufahamu  kuhusu ushiriki wa Tanzania katika  kazi za kulinda amani zinazosimamiwa na Umoja wa Mataifa, akabainisha kwamba wabunge hao wanapashwa pia kufahamu kinachoendelea katika operesheni hizo.

Alisema ni muhimu pia wakafahamu hali ya wanajeshi  wa Tanzania, Polisi na Askari Magereza walio katika operesheni hizo ili kujifunza manufaa ya kiulinzi na uzoefu unaotokana na wanajeshi wa Tanzania kushiriki operesheni hizo.


Akielezea alichojifunza katika utumishi wake wa miaka mitano na kama Naibu Katibu Mkuu wa UN, Migiro alisema: “Yapo mengi ambayo nimejifunza,  lakini kwa  ufupi  tu niseme  nimejifunza,  uadilifu,  uwajibikaji,  kujituma, uzalendo, utii, kujiamini, matumizi sahihi ya yenye tija  ya raslimali,  kuthamini muda wa kazi, ushirikiano wa pamoja na maelewano.”