WANACHAMA
wa Chama cha Mapinduzi (CCM) kijiji cha Isunura wilayani Mbarali Mkoani Mbeya,
wamekataa kufanya uchaguzi wa Mabalozi wa chama hicho kwa madai kuwa viongozi
wao ngazi ya wilaya ya Serikali ya wilaya hiyo kushindwa kuwaunga mkono
wananchi wa kijiji hicho kuwajibika katika kata Mawindi.
Wakizungumza na waandishi wa habari waliofika
kijijini hapo, wamesema kuwa mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu kutokana na
maslahi ya kiutawala kwa viongozi wa Serikali na chama hicho kwa
kuendelea kuwalazimisha wananchi wa kijiji hicho kutaka kuwapeleka katika kata
Mpya ya Igava ambapo wananchi hawaitaki wakitaka kuendelea kuwajibika katika
kata yao ya zamani ya Mawindi.
Wamesema kuwa wao hawakufanya uchaguzi huo wa
mabalozi uliofanyika mwezi mei mwaka huu nchini kote kwa madai kuwa viongozi wa
chama hicho pia wamaeonekana kuwa na usaliti kwa wanachama wake ambapo umekuwa
ukiwageuka kila wanapo kwenda kutoa malamaliko yao kwa vielelezo.
Wamesema hawataki kuwajibika katika kata ya Igava
kutokana na ramani na miundombinu iliyopo lakini Serikali imekuwa
ikiwalazimisha kwa muda mrefu sasa.
Mwenyekiti wa tawi la Isunura Chesco Mduba alisema
kilichowapelekea kukataa kufanya uchaguzi wa mabalozi kijijini hapo ni kutokana
na viongozi wa serikali na wa CCM kuwapuuza wananchi kuhusu mpaka huo huku
wakiendelea kuwalazimisha.
Amebainisha kuwa mgogoro huo ulianza mwaka 2010
baada ya kata ya Mawindi kugawanywa na kupatikana kata tatu ambazo ni kata ya
Igava, Ipwani na Mawindi yenyewe huku kukiwa na vijiji vitano kila kata. Amesema
kufuatia hali hiyo kijiji cha Isunura kinapaswa kuwa kata ya Mawindi ili
kukamilisha vijiji vitano lakini kutokana na baadhi ya watu kutoka kijiji cha
Isunura kutaka madaraka ya uongozi wanataka kulazimisha kukipeleka kijiji hicho
kata ya Igava ambyo kwa sasa ina vijiji vitano huku kata ya Mawindi ikiwa na
vijiji vinne.
Mbali na kukataa kufanya uchaguzi wa mabalozi katika
kijiji hicho ambacho kingekuwa na jumla ya mabalozi 25, viongozi wa chama hicho
na wafuasi wake walisema kuwa wanaandaa utaratibu wa kwenda ofisi ya Katibu wa
CCM mkoa wa Mbeya kueleza yanayowasibu.
Hata hivyo imebainika kuwa Mwenyekiti wa CCM mkoa wa
Mbeya Nawaab Mulla anatokea wilayani Mbarali lakini hajui mambo mengi
yanayokikabili chama chake wilayani humo na hata baadhi ya wilaya anazoziongoza
kwa sasa hali inayomwakikishia kutoweza kutetea nafasi yake katika uchaguzi
unaotarajiwa kufanyika Mwezi Agosti Mwaka huu.
