Jana na juzi habari ya Dogo Janja
kufukuzwa Tip Top Connection imekuwa gumzo.
Kila upande wa wanaouhusika kwenye sakata hili, yaani yeye Dogo Janja na Madee ambaye ndiye aliyehusika kumleta Tip Top na kukabidhiwa na wazazi wake baada ya kumtoa Arusha na kumleta Dar es Salaam, unaongea la kwake.
Kutokana na kutofautiana kwa maelezo kwa pande hizi mbili mashabiki wameshindwa waamini lipi!
Tip Top Connection wanadai kuwa wamefikia uamuzi wa kumrudisha kwao Dogo Janja ambaye jina lake halisi ni Abdul kutokana na mtoto huyo kuwa mtoro shuleni na kulewa sifa.
Lakini kwa mujibu wa maelezo ambayo tuliyapata kutoka kwake mwenyewe Dogo ni kuwa Tip Top walikuwa wanamtumia kimaslahi zaidi kwa kumlipa kidogo kutoka kwenye kile anacholipwa kwenye show zake.
Mtoto huyo aliyekuwa anasoma kidato cha pili kwenye shule ya Makongo, anasema maisha yalikuwa magumu licha ya kila show aliyofanya kulipwa sio chini ya shilingi milioni moja na yeye kuambulia laki na ushee.
