POLISI WAKIDAIWA KUMUUA MTUKUMIWA

ASKARI wawili wa Kituo cha Polisi mjini Iringa wameingia matatani wakituhumiwa kusababisha kifo cha Msimbe Selemani (25), baada ya kumpiga na kumjeruhi vibaya sehemu zake mbalimbali za mwili wake.

Ndugu wa marehemu Selemani, wamekataa kuuchukua mwili wake kutoka katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa wakidai kwamba ndugu yao alikuwa mzima mwenye nguvu zake zote wakati akikamatwa na askari hao.


Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa Evarist Mangalla jana, inaonesha kwamba Selemani anayetuhumiwa kwa makosa ya unyang’anyi kwa kutumia silaha alikufa saa saba usiku wa kuamkia Aprili 10.


Kamanda Mangalla alisema mtuhumiwa huyo alikufa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa wakati akipatiwa matibabu baada ya kupata kipigo kikali kutoka kwa watu wenye hasira kali kwa sababu ya makosa yake.


Hata hivyo taarifa ya Kamanda Mangalla imetofautiana na ile iliyotolewa jana na Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Iringa, Dk. Deogratius Manyama inayoonesha kwamba Selemani alifikishwa na askari Polisi katika hospitali hiyo jana saa 1.15 asubuhi.


Dk. Manyama alisema Selemani aliyekuwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake huku akiwa amevimba sana mdomo wake, alifariki dakika mbili tu baadaye baada ya kufikishwa hospitalini hapo.


Kwa mujibu wa maelezo ya Dk. Manyama, mpaka jana jioni mwili wa marehemu huyo ulikuwa haukufanyiwa uchunguzi wowote.


“Kwa kawaida uchunguzi wa watu waliokufa wakihusishwa na kesi za kipolisi, unatakiwa kufanywa kwa pamoja kwa kushirikiana na Polisi. Hata hivyo hatujafanya uchunguzi wa kifo hicho mpaka sasa kwa sababu tunaendelea kusubiri maelekezo ya Polisi,” alisema.


Akizungumza na waandishi wa habari kwa uchungu jana, msemaji wa familia ya marehemu, Petro Mwani alidai wamestushwa na taarifa za ndugu yao kufa wakati askari hao walimchukua kwa amani walipokwenda kumkamata nyumbani kwake Mtaa wa Isoka A, mjini hapa. “Ndugu yetu alichukuliwa akiwa mzima, tunaamini kifo chake kitakuwa kimesababishwa na askari waliokuja kumkamata kwa sababu Polisi hawataki kutoa maelezo ya kifo chake, hatuko tayari kuuchukua mwili huo, tutajua wenyewe jinsi tutakavyoumaliza msiba huu, kama kumzika mzigo huo watabeba polisi wenyewe,” alidai Mwani huku akilia.