MBUNGE WA CCM KUNYANG’ANYWA VIWANDA ANAVYOMILIKI NA RAIS MAGUFULI

Rais Dkt John Pombe Magufuli mara nyingi husema kuwa yeye si mnafiki na huwa anapenda kusema ukweli kuliko kukaa na vitu ambavyo vitamuumiza moyo. Jana aliendelea kushikilia msimamo huo baada ya kumshukia Mbunge wa Morogoro Mjini, Aziz Abood akimtaka kuvirejesha serikali viwanda alivyobinafsishiwa kama hawezi kuviendeleza.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo jana aliposimama kuzungumza na wananchi katika Kituo cha Mabasi cha Msamvu mkoani Morogoro ambapo alikuwa akisiistiza wafanyabiashara kuviendeleza viwanda walivyonunua kutoka serikali na sio kubadilisha na kufanyia shughuli zao nyingine.
Alisema kwamba, haijalishi aliyenunua kiwanda kutoka serikalini yupo chama gani, lakini kama hawezi kukiendeleza basi akirudishe mwenyewe ili serikali iwape wawekezaji wengine wenye nia na uwezo wa kuviendeleza.
“Narudia wito wangu niliokwishatoa kwamba, wenye viwanda hapa Morogoro ambao wameshindwa kuviendeleza, na leo nataja, akiwemo Mbunge wa hapa CCM, narudia akiwemo Mbunge wa hapa CCM, alibinafsishiwa viwanda vingi, kama ameshindwa kuviendesha, arudishe ili tuwape watu wengine kwa sababu vijana hawa wanakosa ajira. Nazungumza kwa uwazi kwa sababu msema kweli ni mpenzi wa Mungu,” alisema Rais Magufuli.
Wakati Rais akitoa kauli hiyo alipokuwa akirejea Dar es Salaam akitokea Makao Makuu ya Nchi, mjini Dodoma, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage ametoa siku 19 kuanzia leo kwa watu wote waliobianfisishiwa viwanda kuviendeleza ama la watanyang’anywa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mwijage alisema serikali itavichukua viwanda 54 kati ya 156 vilivyobinafsishwa kati ya mwaka 1992 hadi 2004 ambavyo havijaendelezwa ifikapo Agosti 15 mwaka huu.
Waziri Mwijage alisema lengo la kuchukua viwanda hivyo ni ili wapewe wawekezaji wengine wenye nia na uwezo wa kuviendeleza kusudi vitoe ajira kwa vijana wengi ambao wanamaliza vyuo na kukaa mtaani bila ajira.
Katika kuhakikisha viwanda vinafanya kazi, Waziri Mwijage alisema kwa wale wote ambao wanapata ugumu kuviendesha, Taasisi ya Utafiti wa Viwanda na Maendeleo (TIRDO) na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) watatoa msaada ya kitaalamu wa namna bora ya kuviendesha viwanda hivyo.

from Blogger http://ift.tt/2v4esP3
via IFTTT