MAZUNGUMZO KUHUSU FEDHA ZA MAKINIKIA KUANZA KESHO

Mwezi uliopita, Mwenyekiti wa Barrick, Profesa John Thorton alifanya mazungumzo na Rais Dkt. John Magufuli na kukubali kulipa fedha ambazo zitakutwa zilipotea baada ya pande zote mbili kufanya tathmini ila haikutajwa tarehe ya kuanza kwa mazungumzo hayo. Jana alipokuwa akizungumza wilayani Chato katika sherehe za makabidhiano ya nyumba 50 za watumishi wa afya kwa mikoa ya Geita, Simiyu na Kagera zilizojengwa na Taasisi ya Mkapa Foundation kwa kushirikiana na Serikali ya Japan na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Rais Magufuli alisema kuwa mazungumzo hayo yataanza kesho.
“Keshokutwa (Jumatano) mazungumzo yanaanza na wale waliokuwa wanatuibia ibia, na nilishamuagiza Naibu Waziri wa Nishati na Madini kwamba hakuna kutoa leseni mpya katika uchimbaji madini hadi tujipange upya. Atakayetoa leseni na yeye atakwenda na leseni hiyo,” alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa kinachotakiwa katika uchimbaji madini ni faida kwa watu wote, “wageni wachimba na sisi watuachie faida.”
Barrick ni mmiliki mkuu wa kampuni ya Acacia ikiwa na asilimia 63 ya hisa za kampuni hiyo iliyoanza kusafirisha mchanga wa madini tangu mwishoni mwa miaka ya tisini.
Ripoti iliyowasilishwa mwezi uliopita na Profesa Nehemia Osoro kuhusu hasara ya kiuchumi ambayo nchi inaweza kuwa imeipata kutokana na shughuli za kampuni hiyo inaweza kufika shilingi trilioni 489 za kodi na mali kwa miaka 19 iliyopita kwenye biashara hiyo ya madini inayofanywa na Acacia.
Katika fedha hizo, kiwango cha kodi kilitajwa kuwa ni shilingi trilioni 108. Ripoti hii ilitokana na zuio la Rais Magufuli kutaka kuzuia usafirishaji wa makontena yenye mchanga wa madini yaliyokuwa bandarini tayari kwa kusafirishwa kwenda nchi za nje kwa ajili ya uchenjuaji.
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2t9ZHFg
via IFTTT