SABABU ZA VIONGOZI WA TANZANIA KUTOJIUZULU WANAPOKOSEA

Kiongozi muwajibikaji ni yule anayetimiza wajibu wake kwa kuzingatia maslahi ya watu wengine au wananchi anaowaongoza. Kiongozi ana wajibu wa kuhakikisha kuwa anakuwa mfano miongoni mwa jamii au kikundi cha watu anaowaongoza kwa namna anavyofanya au kutokufanya mambo fulani.
Unapokuwa kiongozi utawajibika kwa yale utakayoyasema au kutoyasema au uliyofanya ama ambayo ulitakiwa kuyafanya lakini kwa sababu moja au nyingine hukuyafanya.
Katika makala hii, tutajadili kwanini viongozi wengi wa nchi za Kiafrika tukichukulia mfano Tanzania hawawajibiki kutokana na matendo yao waliyofanya au kutokufanya.
Kuweka mambo sawa kabla ya kuanza mjadala wetu, kuwajibika tunakokuzungumzia hapa ni tukio la kiongozi ama kujiuzulu kutokana na aliyoyafanya au kutofanya au angalau kuomba msamaha kwa wananchi au wafanyakazi wenzake pale anapokosea. Jambo hili tumeliona mara kadhaa katika nchi zilizoendelea ambazo ndizo tunazozitumia kama kielelezo cha kufaulu ama kushindwa kwa demokrasia hapa kwetu. Viongozi hao wamekuwa wakiwajibika hata kwa tuhuma tu ambazo zimekuwa zikiwakabili.
Ule utaratibu wa viongozi kusukumwa na maadili kuachia madaraka wanapokosea ili kuonesha kuguswa kwao na makosa yaliyofanyika haupo tena. Hii inachangiwa na mambo mengi ikiwa ni pamoja na;
Sababu ya kwanza ambayo inawafanya viongozi wengi wa Afrika wasiwajibike kutokana na matendo yao ni umasikini. Umasiki unaotajwa hapa ni ukosefu wa fedha za kutosha kuendesha maisha na shughuli za kila siku za viongozi hao. Viongozi wengi wakifirikiria suala la kujizulu pindi mambo yanapokwenda ndivyo sivyo, jambo ambalo hugonga kwenye akili yao ni, kiasi gani cha fedha (mshahara na marupurupu) watakachopoteza kama waking’atuka madarakani.
Wakati mwingine viongozi hawa hufikiria ni watu wangapi wanawategemea katika familia au koo zao na hivyo wanakuwa hawapo tayari kuachia nafasi ambayo inawaingizia fedha zinazowawezesha kumudu gharama za maisha.
Elimu miongoni mwa wananchi nayo ni sababu kubwa inayochangia viongozi wa Afrika kutowajibika wanapokuwa madarakani. Wananchi kutofahamu nafasi yao katika kuhakikisha kiongozi wao anatimiza wajibu wake imekuwa kama ni mwanya unaotumiwa na viongozi wengi kuwadanganya wananchi kwa vile tu hawajui nafasi yao.
Wananchi wengi hawajui kuwa katika mfumo huu wa demokrasia, wao ndio waajiri wa viongozi na kwamba bila wao viongozi hao wasingekuwa hapo walipo na kwamba kila ambacho kiongozi huyo atakifanya au kutofanya inatakiwa iwe ni kwa kuzingatia maslahi ya watu anaowaongoza. Hii inapelekea hata kiongozi akifanya jambo la maendeleo wanaona kana kwamba wamependelewa au kupewa msaada wakati ni wajibu wa wa kiongozi huyo kuwaletea maendeleo na bila shaka yoyote ile kwamba alichaguliwa kwa ajili ya kuhakikisha maendeleo hayo. Hivyo uelewa mdogo wa wananchi kuhusu masuala ya uongozi kumegeuka mtaji kwa viongozi wengi kuendelea kusalia madarakani hata wanaposhindwa kutimiza majukumu yao.
Utasikia baadhi ya wananchi wanasema: Waziri ajiuzulu kwani yeye ndiye alikuwa anaendesha gari lililoua abiria, au yeye ni nahodha wa meli iliyozama Ziwa Victoria na kuua raia zaidi ya elfu moja. Wao wanaamini kuwa anayepaswa kujiuzulu ni yule tu aliyefanya kosa na si mkuu wake.
Baadhi ya viongozi hukataa kuwajibika ama kwa kuomba msamaha au kujiuzulu kutokana na kuwa na kiburi kinachosababishwa na mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja kiburi cha fedha, usomi unaowafanya wajione wao ndio pekee wanaweza kushika wadhifa fulani na kwamba mtu mwenye elimu chini ya ile aliyonayo yeye hapaswi kuongoza.
Viongozi kama hawa huwa na kiburi kinachowafanya wajione kwamba wao ndio wataalamu pekee wanaoweza kushika nyadhifa fulani na kwamba hata wakiondoka hakuna atakaweza kufanya kama wao. Hii inachangiwa na uhaba wa wataalamu wengi katika nchi za Afrika mfano Tanzania. Uchache wa wataalamu unawafanya waliopo wawe na kiburi.
Viongozi wengi wa Tanzania kutokuwajibika kwao wakati mwingine kunaweza kuelezewa na kutoelewa dhana nzima ya uwajibikaji na namna inavyotakiwa kufanya kazi. Viongozi wengi hudhani kuwa kwa kuomba msamaha au kung’atuka madarakani pale ambapo mambo yanakwenda ndivyo sivyo yatawafanya waonekane ni dhaifu.
Kwao wanaamini kuwa kuendelea kuwa madarakani wakati mambo hayaendi sawa sawa, mfano watu wanakufa au kutekesa, ataonekana amekomaa kiuongozi na kwamba hajakimbia tatizo badala yake anakabiliana nao. Hii haimaanishi kuwa kila tatizo linapotokea kiongozi anatakiwa kuwajibika kwa kujiuzulu, lakini kama tatizo hilo linaichafua serikali na kwa muda limekuwepo na hujachukua hatua yoyote au umechukua hatua lakini hakuna matokeo chanya, ni vyema kumpisha mtu mwingine.
Waswahili husema tabia hujenga mazoea, na hii tunaweza kuitumia kuelezea suala la uwajibikaji katika Taifa hili. Kutokana na viongozi kutokuwa na utamaduni wa kuwajibika pale wanapokosea, tabia hiyo imekuwa ikirithishwa vizazi hadi vizazi na hivyo tunazidi kuwa na viongozi ambao hawana utamaduni huo.
Viongozi wengi wa kitanzania hata wanapojua kuwa wamekosea ama kwa kufanya kitu kwa makusudi au bahati mbaya huendelea kusalia madarakani au kutoomba msamaha. Hii ni kutokana na tabia au aina ya uongozi ambayo tumekuwa tukiirithi kutoka kwa watangulizi wetu kwani wengi husubiri hadi mamlaka za uteuzi ziwaondoe badala ya kuondoka au kuomba radhi ili kulinda heshima yake, heshima ya serikali, taasisi au kampuni anayoiongoza.
Nchini Tanzania, viongozi ambao wamewahi kujiuzulu wenyewe kwa hiyari yao ni wachache sana. Wengi waliojiuzulu bila msukumo wowote/kwa hiyari zao walikuwa chini ya Mwalimu Nyerere ambapo wa kwanza ni Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani miaka ya 1970. Yeye alijiuzulu baada ya kuibuka ripoti za mauaji ya raia katika Mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Mwingine ni Abdallah Natepe ambaye alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani miaka ya 1980. Natepe alijiuzulu baada ya watuhumiwa wa kesi za uhaini waliokuwa katika gereza la Keko Dar es Salaam kutoroka. Natepe alisema kuwa anajiuzulu mara moja na anachukuwa lawama zote kwa tukio hilo kutokea chini ya Wizara yake.
Wa mwisho ambaye alijiuzulu kwa hiyari yake ni aliyekuwa Waziri Mkuu chini ya Rais Jakaya Kikwete, Edward Lowassa baada ya kuhusishwa na kashfa ya Richmond mwaka 2008.
Sababu ya mwisho lakini si ya mwisho kwa umuhimu ni Katiba za nchi nyingi za Afrika. Katiba nyingi za nchi za Afrika hazitoi mazingira rafiki au hazitoi nafasi kabisa kwa wananchi kuweza kuwawajibisha viongozi wao pale wanapokwenda kinyume na sheria, taratibu au kufanya jambo kinyume na tamaduni za Taifa husika.
Mfano kwa Tanzania, Katiba haitoi nafasi kwa wananchi kuwawajibisha wabunge au madiwani waliowachagua wao wenyewe kwa kura zao kabla ya muda wao haujaisha endapo watafanya kazi kinyume na makubalino au kutotimiza ahadi walizotoa. Lakini pia mazingira ya kumuwajibisha Waziri Mkuu wa Rais ni magumu kiasi kwamba hayawezi kufikiwa. Hii imekuwa ikiwalinda viongozi wengi na kuwafanya waendelee kukaa madarakani na wanapokaribia muda wao wa uongozi ndio hujipendekeza na kuwahadaa wananchi ili wawachague tena.
Katika dhana nzima ya uwajibikaji, kiongozi hawajibiki tu kwa yale aliyoyafanya au kutokuyafanya yeye, bali hata kwa yale yaliyofanywa au kutofanywa na watu waliopo chini yake ambao yeye ndio anawaongoza.
Kujiuzulu ni ujasiri ambao unatuma ujumbe kwa wananchi kuwa cheo ulichonacho ni dhamana na kuwa unasikitishwa na kitendo kilichotokea chini ya uangalizi wako wewe kama Waziri, Mkurugenzi, Mbunge, Diwani au kiongozi yeyote.
Kwa kuwataja, hawa ni baadhi ya viongozi ambao walitakiwa kujiuzulu wenyewe lakini walifanya hivyo baada ya misukumo kotoka pande mbalimbali; Andrew Chenge, Nazir Karamagi, Ibrahim Msabaha, William Ngeleja, Prof. Muhongo, Fredrick Werema, Limford Mbona (aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa TRC (TRL sasa)).
 ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2tjjROr
via IFTTT