MAMBO 17 MUHIMU YA KUZINGATIA KUEPUKA MOTO UNAOSABABISHWA NA UMEME MAJUMBANI

Mara kadhaa tumesikia au kuona nyumba na zikiungua na watu kupata hasara za mali na wakati mwingine wenyewe kufariki ama kwa kuungulia ndani ya nyumba au kutokana na mshtukio wa nyumba zao kuungua kutokana na hitilafu ya umeme.
Hitilafu za umeme zinazoweza kupelekea madhara hayo ama zinaweza kusababishwa kutokana na matumizi ya nyumbani au mfumo wa umeme wenyewe. Hivyo ni vyema kuchukua tahadhari kabla hayo hayajatokea.

Hapa chini ni mambo muhimu ya kuzingatia kuepuka matukio ya moto unaosababishwa na umeme majumbani;

  1. Hakikisha utandazaji nyaya (wiring) katika nyumba inafanywa na mkandarasi aliyesajiliwa na serikali kwa wao huwa na ujuzi wa kutosha kuweza kufahamu kifaa gani kinahitajika sehemu gani.
  2. Hakikisha vifaa vyote vinavyofungwa katika nyumba yako (nyaya, soketi, swichi, saketi breka) vimethibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Vifaa ambavyo havijathibitishwa si salama kwa matumizi
  3. Hakikisha waya wa ethi umethibitwa na TBS na umechimbiwa chini ardhini inavyotakiwa
  4. Hakikisha unapotumia pasi usiiache ikiwaka ukande kufanya kazi nyingine. Pia vifaa vingine kama jiko la umeme, hita, hakikisha unazitoa au kuzima swichi mara baada ya kuzitumia ndipo uendelee na mambo mengine.
  5. Usinyooshe nguo juu ya kitanda kwa kutumia pasi ya umeme.
  6. Epuka kutumia ‘extension cables’ kwa kudumu. Zitumike kw adharura na pia usiziweke kwenye mazulia.
  7. Usichaji simu au kutumia kompyuta mpakato (laptops) ukiwa umeziweka kitandani.
  8. Usichomeke vitu vingi vinavyotumia umeme katika sakiti moja, mfano redio, runinga, jokofu, pasi.
  9. Usiweke mapazia marefu dirishani yanayofunika soketi za umeme. Ni heri kuihamisha ikaka sehemu ya wazi kuliko kuifunika na pazia.
  10. Unashauriwa kutumia mapazia yasiyoshika moto kwa urahisi, mfano mapazi ya pamba.
  11. Hakikisha godoro la kitanda chako haligusani na swichi au soketi ndani ya nyumba yako.
  12. Makochi ndani ya nyumba yako na samani nyingine za ndani zisigusane na swichi au soketi yeyote ili isiwe rahisi kushika moto tatizo linapotokea. Ziweke angalau umbali wa inchi sita.
  13. Kama fyuzi ya umeme itakatika au soketi breka itajizima yenyewe, hakikisha umemuita fundi kuja kukagua tatizo. Usiweke fyuzi nyingine au kuwasha soketi breka.
  14. Hakikisha unamuita mkandarasi aliyesajiliwa kupitia mfumo wote wa umeme kwenye nyumba hasa maungio kila baada ya miaka mitano.
  15. Usiongoze vitu vinavyotumia umeme mwingi kama viyoyozi bila kuwahusisha wakandarasi waliosajiliwa kuangalia uwezo wa umeme wako kuhimili mzigo unaouongeza.
  16. Usiunganishe umeme kutoka nyumba moja kwenda nyingine au kwenda kwenye banda la kuku bila kuwahusisha wakandarasi waliosajiliwa.
  17. Ikitokea hitilafu yoyote ya umeme kuanzia kwenye mita ya TANESCO, braketi nguzo ya kwenye laini ya umeme, toa taarifa kwenye ofisi ya TANESCO iliyokaribu na wewe kwa kutumia namba za dharura.

from Blogger http://ift.tt/2rQbFov
via IFTTT