MADHARA YA KIAFYA YA KUVAA NGUO ZA KUBANA

Kwa msaada wa viguo vya kubana na vivazi vyote vinavyochonga shepu ya mwili, wengi mchana huonekana na maumbile mazuri yanayovutia kuangalia na usiku wanarudi kwenye miili yao iliyotepweta baada ya kuzivua nguo zao.
Hatuoni tabu yoyote hata kujipaka mafuta ikibidi mradi tuweke kuingia kwenye jinzi za kubana au hata kuvaa ‘skini taiti’ mbili, vyovyote iwavyo ili mradi tuonekane wembamba kuliko tulivyo, tuonekane wazuri na wenye mvuto kuliko tulivyo na nyakati nyingine kwakuwa tunataka tuonekane vijana kuliko tulivyo.
Kama unaihusudu sana jinzi yako ya kubana, bila shaka ushawahi kupata tatizo la mwili kupatwa na ganzi kuanzia mapajani na kupoteza hisia kabisa kwenye mguu mzima mpaka chini. Madaktari wanaiita hali hii kwa jina la kitaalamu la meralgia paresthetica ambayo hutokea kwa sababu ya kukandamiza kwa muda mrefu mishipa ya neva za fahamu inayotoka kwenye kiunoni ambayo kazi yake ni kuleta hisia kwenye mapaja.
Mwili wa binadamu unatoa ishara fulani kama nguo au mapambo fulani tuliyovaa yanabana sana hata kama tukijidai kudharau tunayoyaona kwa macho yetu kupitia kioo ukiwa unajikagua kama umependeza ama la. Yafuatayo ni baadhi tu ya madhara ya kiafya unayoweza kuyapata kutokana na kuvaa nguo zinazobana mwili:
Ugumba
Dkt. George Bwesigye, daktari katika hospitali ya Najeera anatoa maelezo ambayo yanaweza kuwatisha wanaume wengi. “Kokwa zinazotengeneza mbegu za kiume zinatakiwa ziwe kwenye joto la chini tofauti na joto la mwili, ndio sababu zikawa nje ya mwili. Kwa hali hii, zinakuwa na uwezo wa kuzalisha mbegu za kiume kwa wingi. Kwahiyo, kuzibana na nguo kunazuia au kupunguza kwa kiasi kikubwa kazi yake hii ya msingi na huweza kusababisha ugumba.”
Maambukizi
Anasema kuwa chupi zinazobana husababisha joto linaloleta unyevu kwenye eneo hilo nyeti. Unyevu katika sehemu hiyo husababisha vjidudu vya fangasi kwa wanaume au utandu wa vijidudu unaosababisha muwasho na maambukizi kwa wanawake.
Mzunguko mdogo wa damu
Nguo za kubana zinazuia mzunguko unaotakiwa wa damu, ikizuia mzunguko wake wa kawaida wa kupeleka damu na kuirudisha kwenye moyo kwa ajili ya kutumika tena mwilini.
Hili linaleta maumivu, uvimbe au kuvimba/kupinda kwa mishipa ya damu ya miguu kutokana na presha kubwa inayopelekwa sehemu ya chini ya mwili. Kama una tatizo la kuwa na mafuta mengi mwilini, kuvaa nguo za kubana kunaliongeza tatizo hilo kwakuwa mzunguko wako wa damu utaathirika zaidi.
Matatizo ya mmeng’enyo wa chakula
Bwesigye anaendelea kueleza kuwa suruali na mikanda ambavyo vinabana sana tumbo vinakuwa vinalizuia tumbo kutanuka jambo ambalo ni la muhimu sana kwa ajili ya usagaji wa chakula ulichokula.
“Kwakuwa mfumo wa usagaji chakula haufanyi kazi sawa sawa, mtu atajikuta anapata viungulia na kujaa kwa kemikali tumboni, na matatizo mengine mengi,” amesema.
Maambukizo ya njia ya mkojo (UTI)
Mbunifu wa mavazi kwa watu mashuhuri, Solomon Tazibone amesema kuwa wanawake wanaovaa nguo za kubana mara nyingi sana hukwepa kutumia vyoo vya kadamnasi, ambavyo vinahatarisha wanawake wengi sana kupata maambukizi ya njia ya mkojo.
“Si rahisi kutua nguo zilizokubana sana hasa kwenye vyoo vinavyotumiwa na watu wengi. Kwahiyo wanawake wengi hujikuta wakizuia haja ndogo kwa saa kadhaa wakisubiri kwenda sehemu walizozizoea na salama kwao kama majumbani mwao,” anasema.
“Tatizo kubwa zaidi ni pale nguo hizi zinapovaliwa na mabinti wadogo. Tunaweza tukabisha lakini hali halisi ni kwamba wanaume wanapenda kuona vitu vinavyowavutia na hawatasita kumuita mtoto wa miaka 11 aliyevaa kaptura au hata kumuangalia kwa matamanio.
Kama wazazi ni jukumu lenu kuwalinda watoto wenu hata kama utaitwa mshamba au mkoloni.
 ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2sDCO0G
via IFTTT