INASIKITISHA:Mwanafunzi wa Miaka 13 Abakwa Korongoni Hadi Kufa

Mwanafunzi wa darasa la sita mwenye umri wa miaka 13 anayesoma Shule ya Msingi Kipanga wilayani Tanganyika mkoa wa Katavi, amebakwa hadi kufa na watu wasiojulikana, ambao waliutupa mwili wake korongoni.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi, Benedict Mapujila alisema kitendo hicho cha kikatili ni cha juzi ya saa 11:30 kijijini humo . Alisema siku ya tukio hilo, mwanafunzi huyo wa kike aliondoka nyumbani kwao kama kawaida yake kwenda shule.
Hata hivyo, hakurudi tena kwao na kusababisha wasiwasi mkubwa kwa wazazi wake, kwa kuwa hakuwa na tabia ya kuchelewa kurudi nyumbani.
Wazazi wake walikuwa na wasiwasi mkubwa kwa binti yao kuchelewa kurudi nyumbani, hivyo waliamua kutoa taarifa kwa uongozi wa kijiji chao.
Viongozi hao wa kijiji na wananchi, walianza kumsaka binti huyo kwenye maeneo mbalimbali bila kukata tamaa.
“Ilipofika saa kumi na moja na nusu ya jioni waliukuta mwili wa mwanafunzi huyo ukiwa umetupwa korongoni na kubaini kuwa alikuwa amebakwa huku sehemu zake za siri zikiwa zimeharibika vibaya,“ alisisitiza .
Alisema chanzo cha kifo cha mwanafunzi huyo wa kike, kilisababishwa na kuvuja kwa damu nyingi baada ya kufanyiwa ukatili huo na watu ambao hawajafahamika.
Kamanda huyo alisema hakuna aliyekamatwa kuhusu tukio hilo na jeshi la polisi linaendelea kusaka wahalifu hao.
Alisema baada ya kuufanyia uchunguzi wa kitabibu, mwili wa marehemu ulikabidhiwa kwa ndugu kwa ajili ya maandalizi ya maziko yake.
ASANTE KWA KUTEMBELEA MTANDAO WETU!!

from Blogger http://ift.tt/2snV0M0
via IFTTT