Mjane Aangua Kilio Hospitali Baada ya Kujifungua Mapacha 4, Asema Hawezi Kuwalea

Hali ya umaskini pamoja na kufikiria namna ya kuwalea watoto wanane baada ya kujifungua wanne jana imemtoa chozi mkazi wa Yombo, Ashura Shaibu (37).
“Lakini nilipatwa na mshtuko baada ya kujifungua watoto wanne kwani ni jambo ambalo sikulitegemea,” alisema
Ashura alijifungua watoto hao katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke, lakini mzazi huyo hakufurahia tukio hilo kwa kuwa haikuwa matarajio yake ikizingatiwa kwamba familia yake ni maskini.
“Nilifurahi kusikia nimejifungua watoto wanne ingawa mume wangu amekwishafariki na sina mtu wa kunisaidia kwani hata mama yangu anaishi mbali na mimi na wazazi wa mume wangu wamekwishafariki,” alisema Ashura.
Mume wa mama huyo alifariki Desemba mwaka jana wakati akiwa mjamzito.
Alisema hali yake kiuchumi si nzuri kwani kabla ya kupata ujauzito, alikuwa akijishughulisha na biashara ndogo ndogo katika eneo la nyumba yake lakini mimba ilipofikisha miezi minne, alichoka na kushindwa kumudu shughuli zake na biashara.
“Nina maisha magumu, nina watoto wanane, sijui namna nitakavyowalea,” alisema.
Muuguzi katika wodi ya watoto wenye upungufu wa uzito Hadija Kamote anasema mama huyo alijifungua kwa njia ya kawaida ila watoto walionekana kuwa na uzito pungufu.
“Watoto wamezaliwa wa kiume watatu na wa kike mmoja. Wa kwanza ana uzito wa kilo 2 na gramu 300,wa pili ana uzito wa kilo 1 na gramu 900, wa tatu ana uzito wa kilo 1 na gramu 700 na mtoto wa nne ana uzito wa kilo 1 na gramu 300,” alisema Kamote.
Muuguzi Mkuu katika Hospitali ya Temeke Deodata Msoma alisema mama huyo baada ya kujifungua alionekana kukata tamaa na kuanza kulaumu kwanini amepewa watoto hao.
“Ilibidi tufanye kazi ya kumtuliza na kumtia moyo kuwa asikate tamaa na kumuambia wapo watu watakaomsaidia huku tukijaribu kufanya vitu vitakavyo mfurahisha na kurudisha tabasamu usoni kwake,” alisema Deodata. Atakayeguswa kumsaidia Ashura afanye hivyo kwa kutumia namba 0783- 287929.
Chanzo: Mwananchi

from Blogger http://ift.tt/2s6Nstk
via IFTTT