ZANZIBAR INAZIDI KUKUA KWA KASI YA KIMAENDELEO



Balozi wa Korea Kusini Nchini Tanzania Bwana Song Geum Yong amesema Zanzibar inazidi kubadilika Kimaendeleo kutokana na kasi kubwa ya miundombinu inayoendelea kuwekwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ikiungwa mkono na Mataifa na Taasisi washirika wa Maendeleo.

Amesema Taasisi na Makampuni ya Korea yanafurahia mabadiliko hayo na kuamua kusaidia ujenzi wa Miradi ya Kielimu akiutolea mfano ule wa Skuli ya Sekondari ya Kwarara uliomalizika hivi karibuni ili kuipa nguvu zaidi Sekta ya Elimu Zanzibar ambayo ndio kichwa cha maendeleo hayo.

Balozi Song Geum Yong alieleza hayo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar aliyekuwepo Visiwani Zanzibar katika uzinduzi wa Skuli hiyo pamoja na kuhudhuria maadhimisho ya sherehe za kutimia miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema anapata faraja kuona kuwa ujenzi wa Skuli hiyo uliopata msaada kutoka Shirika la Maendeleo ya Korea { KOICA }, Good Neighbors, Shirika la Utangazaji la Korea { SBS } na Taasisi ya Wasanifu Majengo ya Korea umekwenda sambamba na ujenzi wa Kituo cha Habari cha Kimataifa cha Tumaini.

Balozi Song alieleza kwamba Kituo hicho cha kurekodia Matangazo ya Redio na Televisheni cha Tumaini kilichoanzishwa kwenye Skuli hiyo ya Sekondari Kwarara kwa kiasi kikubwa kitasaidia kutoa Taaluma kwa Wanafunzi pamoja na Wananchi wa sehemu mbali mbali hapa Zanzibar.

Akitoa shukrani zake kwa misaada mbali mbali inayotolewa na Korea kwa Tanzania na Zanzibar kwa jumla Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema Serikali inakusudia kujenga Bara bara ya lami inayoingia kutoka bara bara Kuu hadi kwenye Skuli hiyo ili kuwaondoshea usumbufu wa Mawasiliano Wananchi na Wanafunzi wa eneo hilo.

Balozi Seif alisema Korea ya Kusini inastahiki kupongezwa kwa jitihada zake za kuunga mkono maendeleo ya Zanzibar, lakini hata hivyo alimshauri Balozi Song kutumia maarifa yake katika kuzishawishi Taasisi na Makampuni ya nchi yake kuendelea kuelekeza nguvu zao katika uwekezaji wa sekta tofauti ikiwemo ile ya usafiri wa Baharini.

Alisema sekta ya Kilimo Zanzibar hasa katika upande wa umwagiliaji pia inastahiki kuungwa mkono zaidi ili kuwaongezea nguvu za uzalishaji Wakulima kwa vile zaidi ya asilima 80 ya Wananchi wa Visiwa vya Zanzibar wanaendesha maisha yao kwa kutegemea sekta hiyo.

Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Balozi Song Kati kati akielezea faraja yake kwa Balozi Seif kutokana na Makampuni na Taasisi za nchi yake kuonyesha azma ya kutaka kusadia maendeleo ya Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.Balozi Seif Kushoto akisisitiza malengo ya SMZ katika kuimarisha miundombinu ya sekta mbali mbali nchini ili kuwajengea maisha bora wananchi wake.Balozi Seif Kushoto akimpatia zawadi ya vyakula vya viungo Balozi wa Korea Kusini Bwana Song mara baada ya kumaliza mazungumzo yao Oisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.Picha na – OPMR – ZNZ.Balozi wa Korea Nchini Tanzania Bwana Song Geum Yong akisalimiana na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Vuga Mjini Zanzibar walipokutana kwa kubadilishana mawazo.
Michuzi