Ulaya yaigeukia Uturuki kusaidia kuzuia wimbi la wakimbizi


Viongozi wa Umoja wa Ulaya na Uturuki wanatazamiwa kuandaa mpango wa kuisadia Uturuki katika kukabiliana na mgogoro wa wakimbizi kutoka Syria na Iraq na kuzuia idadi ya watu wanaokimbilia barani Ulaya.
Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker na rais wa bunge la Ulaya Donald Tusk
Rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker na rais wa bunge la Ulaya Donald Tusk
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan anakutana leo hii mjini Brussels na kwa mazungumzo na rais wa Umoja wa Ulaya Donald Tusk na rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Junker na rais wa bunge la Ulaya Martin Schulz.
Umoja wa Ulaya unataka kupata makubaliano yatakapata imani ya pande zote mbili ambayo ni muhimu hasa ikizingatiwa dhima kuu iliyobebwa na Uturuki katika suala zima la mgogoro wa wakimbizi amesema msemaji wa tume ya Umoja wa Ulaya Margaritis Schinas.Uturuki imewapokea kiasi wakimbizi milioni 2 wengi wakitokea Syria na Iraq.Mamia kwa maelfu ya watu wanayoyakimbia mapigano na umasikini wamekuwa wakivuka mpaka kutoka Uturuki na kuingia nchini Ugiriki wakiwa na matumaini ya kupata maisha bora barani Ulaya.
Rais Recep Tayyip Erdogan akiwa Brussels
Rais Recep Tayyip Erdogan akiwa Brussels
Umoja wa Ulaya lakini sasa unaitaka Uturuki kuchukua juhudi zaidi kuwazuia wakimbizi hao kuingia Ulaya.Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan akihutubia umati wa watu huko Strassburg nchini Ufaransa hapo jana kabla ya kuelekea Brussels alizikosoa nchi za Umoja wa Ulaya kuhusiana na sera zao juu ya uhamiaji.
''Sisi tuna sera za kufungua milango yetu na sera zetu zitaendelea kuwa hivyo.Nawatolea mwito Umoja wa Ulaya kutokea hapa nilipo.Je hakuna kitu chochote kwa watu hawa kinachozungumzia haki za binadamu katika mkataba wao?hamjawahi kusoma mkataba wa haki za binadamu?Ni kwanini mlianzisha tume kwa ajili ya wahamiaji katika Umoja wa Mataifa?Kazi ya tume hizo ni nini?
Rais Erdogan alizishutumu nchi za Umoja wa Ulaya kwa kuwatia msukumo wakimbizi kujitosa kwenye kina cha bahari ya Mideterrenia kwa ajili ya kutorokea Ulaya. Akishangiliwa na umati wa mamia ya watu waliohudhuria mkutano huo wa hadhara mjini Strassburg wakosoaji wamemtuhumu kwa upande mwingiune kwa kuandaa mikutano ya umma nchini mwake na hata Ulaya kwa lengo la kukipigia debe chama tawala kuelekea uchaguzi wa Novemba Mosi.
Wakimbizi wa Syria wanaoishi kwenye makambi Uturuki
Wakimbizi wa Syria wanaoishi kwenye makambi Uturuki
Umoja wa Ulaya umepanga kuipatia Uturuki hadi Euro Billioni moja kwa ajili ya kuisadia nchi hiyo kuwashughulikia wakimbizi pamoja na fedha nyingine za kusaidia kuwasajili wakimbizi wapya na kuboresha hali yao ya maisha nchini Uturuki huu ukiwa ni mkakati maalum wa kuzuia wimbi la wakimbizi kuingia katika nchi za Umoja huo.
Halikadhalika Umoja wa Ulaya unaitaka Uturuki kuisadia Ugiriki kulinda mpaka wake baina ya nchi hizo mbili kwa kupiga doria kwa pamoja katika bahari yake.Ingawa hadi sasa Umoja wa Ulaya haujaweka wazi kuhusu mpango wake huo mpya wa kukabiliana na wimbi la wakimbizi tayari mkuu wa shirika la kutetea haki za wakimbizi nchini Ujerumani Guenter Burkhard amekemea juu ya kuchukuliwa hatua yoyote ya kuufunga mpaka wa bahari kati ya Ugiriki na Uturuki akisema ni sawa na kutangaza kuishiwa kwa maadili ya kiutu hasa kutokana na sheria za kimataifa kupinga hatua ya kukataliwa kwa watu wanaotafuta hifadhi.
Mwandishi Saumu Mwasimba
Mhariri:Josephat Charo