WACHUNGAJI 200, MAASKOFU 50 KUUNGANA NA JK TAMASHA LA KUOMBEA AMANI




Na Mwandishi Wetu


VIONGOZI  wa kiroho 250 wa madhehebu mbalimbali ya dini ya kikristo wamealikwa kushiriki kwenye Tamasha la Amani Jumapili wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama (Pichani) ilieleza kuwa kati ya viongozi hao 200 ni Wachungaji na 50 ni Maaskofu.

“Idadi inaweza kuwa kubwa zaidi, lakini hadi sasa niseme hao ndiyo ambao tuna uhakika nao watashiriki katika Tamasha la Amani Jumapili, ambapo mgeni rasmi atakuwa Rais Jakaya Kikwete.

“Maandalizi kuhusu tamasha yanaenda vizuri na nina imani Watanzania na wapenda amani wote waliopo hapa nchini hata kama sio raia wa hapa watajitokeza kwa wingi siku hiyo.

“Ni tamasha ambalo dhamira yake ni kuomba kwa Mungu tuweze kupita kwa usalama kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu,” alisema Msama katika taarifa hiyo.

Tamasha hilo lenye dhamira ya kuombea nchi amani kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani litahusisha wasanii mbalimbali wa nyimbo za Injili kutoka Tanzania na nje ya Tanzania.

Baadhi ya wasanii wa nje waliothibitisha kushiriki ni Sipho Makhabane, Sohly Mahlangu wa Afrika Kusini, Sarah K wa Kenya, Ephraim Sekeleti wa Zambia na Solomon Mukubwa raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi Kenya.

Baadhi ya wasanii wa Tanzania watakaoshiriki ni Rose Muhando, Upendo Nkone, John Lissu, Upendo Kilahiro, Boniface Mwaitege , kwaya ya St. Andrew ya Dodoma na kwaya ya Uinjilisti Kijitonyama.
By MichuziBlog