Bulaya adaiwa kupeleka Mabaunsa Bunda.

BAADHI ya wanasiasa wa Jimbo la Bunda Mjini wanadaiwa kuibua wasiwasi jimboni humo baada ya kudaiwa kukodi mabaunsa kutoka nchi jirani kuwakabili watu wa vyama vingine wanaopinga katika kampeni.

Miongoni mwa wanaodaiwa kukodi watu hao, ni wagombea wa nafasi za ubunge katika jimbo hilo na alitajwa mgombea ubunge wa Chadema, Ester Bulaya. Hata hivyo, Bulaya alikanusha tukio la kuwepo kwa mabaunsa kutoka nchi jirani na kufafanua kuwa walinzi wa chama hicho ni raia wa hapa nchini na kusema kuwa wala hawana silaha zozote kama inavyodaiwa na upande wa pili (Chama Cha Mapinduzi).
Ujio wa watu hayo jimboni humu unahusishwa na vitendo vya utekaji vilivyoibuka hapa, ambapo juzi mtu aliyejulikana kwa jina la Charles Yapanda mkazi wa kijiji cha Kunzugu, wilayani hapa alitekwa baada ya kuingizwa kwenye gari ya watuhumiwa hao hadi kwenye hoteli moja iliyoko eneo la Bunda stoo, mjini Bunda.
Ilidawa baada ya kumfika katika hoteli moja walimofikia, walimpiga Yapanda wakimtuhumu kutowaunga mkono na badala yake anamuunga mgombea mwingine ambaye ni mpinzani wao.
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo.
“Huo ni uhalifu hauwezi kuteka mtu na kumshambulia eti sababu hawaungi mkono mtu unayemtaka,” alisema Mirumbe.
Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Philipo Kalangi, jana alithibitisha kwa njia ya simu kukamatwa kwa watu hao na kwamba atatoa taarifa kamili baada ya uchunguzi wake kukamilika.
Alisema taarifa alizonazo ni kwamba Yapanda alishambuliwa na kujeruhiwa kichwani na amekwishafungua kesi polisi na upelelezi bado unaendelea.
Tuhuma hizo zinahusishwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Polisi ilisema pia kuwa hivi karibuni watu wasiojulikana waliwavamia wanakwaya wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kumshambulia mwanamke moja aliyejulikana kwa jina la Lucy Yohana (53) aliyeshindwakukimbia kutokana na umri wake kuwa mkubwa, ambapo kesi hiyo pia iko polisi.
Source: Habarileo