JK amvaa Lowassa


JKZawadi
Rais Kikwete akifurahia trekta alilozawadiwa na wafanyakazi wa wizara ya ujenzi kwenye sherehe za kumuaga zilizofanyika Mnazimmoja, Dar es Salaam, jana
Rais Jakaya Kikwete, amefananisha nguvu inayotumiwa na upande wa pili katika mbio za kupata urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni sawa na moto wa mabua ambao ukiwaka haudumu.
Bila kutaja moja kwa moja upande huo, alisema urais haupatikani kwa kulazimisha. Rais Kikwete, alisema hayo jana wakati alipokuwa akiagwa na wafanyakazi wa Wizara ya Ujenzi.
Akizungumza na wafanyakazi hao, Rais Kikwete alisisitiza kuwa rais ajaye atapatikana kwa uwezo wa Mungu na siyo kwa kulazimisha: “Ninaomba rais ajaye awe bora kuliko mimi, kwani akipatikana wa kiwango changu nchi itadumaa,” alisema Kikwte.
Watumishi hao wa Wizara ya Ujenzi walimzawadia trekta na lori ili atumie kwa shughuli za kilimo na kubebea mazao baada ya kustaafu mwishoni mwa mwaka huu.
“Matumaini yangu mtaendelea kufanya kazi vizuri na uongozi unaokuja. Mungu yupo nasi, taifa litampata kiongozi bila kulazimisha kwani hata ukiyalazimisha hayatakuwa,” alisema Rais Kikwete.
Alisema kuwa ili kuwa rais mtu hahitaji kuwa na shahada nyingi kinachotakiwa ni kiongozi ambaye anaweza kuunganisha watu na kuweka malengo.
Akizungumzia wizara hiyo, alisema sekta ya miundombinu ni ya muhimu kwani uchumi hauwezi kukua wala kuimarika bila kuendeleza njia za mawasiliano: “Hakuna kinachoweza kufanikiwa kama hataimarisha barabara, reli, usafiri wa angani na wa majini.”
Alisema kwa upande wa barabara serikali ya awamu yake ilipanga kuwa zote ziwe na lami. Kadhalika kuziunganisha barabara zote za mikoani tena ziwe za lami, kuimarisha njia za vijijini ili ziweze kupitika wakati wote na sasa anajivunia mafanikio kwa vile kazi hizo zimefanyika.
Alieleza kuwa maeneo ambayo hayajakamilika makandarasi wapo kazini kuendelea na ujenzi. “Kazi iliyobakia ni ndogo hivyo rais ajaye atahakikisha kazi inamalizika kama itakuwa haijamalizika hadi kufikia kipindi hicho.”
Aliwaambia wafanyakazi hao ambao wanakuwa wa kwanza kumuaga rais, kuwa anafuraha kumaliza muda wake akiiacha sekta ya ujenzi katika hali nzuri yenye mafanikio makubwa.
“Katika wizara iliyonifanya nilale usingizi usio wa mang’amung’amu ni hii. Dk Magufuli pamoja na kwamba amesomea masuala ya sayansi amefahamu mambo mengi zaidi hata yasiyokuwa ya kisayansi,” alisema Kikwete.
Alisema kazi yake kuwa kiongozi bora anafuatilia mambo na kuhakikisha yanatekelezwa, hivyo taifa likimpata mtu kama Dk John Magufuli, ambaye ni Waziri wa Ujenzi litanufaika.
“Kila wizara aliyopelekwa aliimudu na alifanya vizuri kuna wakati mwingine walisema wizara fulani ina matatizo labda apelekwe…Jambo hilo lisingewezekana kumpeleka Dk Magufuli kila wizara,” alisema Rais Kikwete.
Alimsifu kuwa hakupenda sifa kwani kuna baadhi ya mawaziri wakifanya jambo wanajisifia kuwa ametekeleza ila kwa upande wa Dk Magufuli amekuwa akiyahusisha mafanikio na kazi za Rais Kikwete.
MAGUFULI
Akizungumza katika tafrija hiyo , Dk Magufuli alisema katika miaka 15 ya utumishi wa wizara hiyo imejenga barabara zilizounganisha mikoa yote kwa kiwango cha lami.
Aliziomba taasisi zote zilizochini ya Wizara ya Ujenzi kumuunga mkono kwenye kampeni ili kufanikisha kuchaguliwa kuiongoza Tanzania.
Dk Magufuli, naye alimtupia kijembe mmoja wa wagombea urais kupitia vyama vya upinzani, aliyesema kuwa akiingia Ikulu atawasaidia waendesha bodaboda, akisema mtu huyo kasahau kujiuliza vyombo hivyo vya usafiri vililetwa na nani.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI