Kiongozi wa Chechnya Ramzan Kadyrov amewataka wanaume kuwazuia wake zao kutumia mtandao wa kijamii wa WhatsApp baada ya mada ya ndoa ya lazima kusambaa katika ujumbe mfupi wa simu.
Kadyrov amekaririwa akisema "wafungie ndani, msiwaache wakatoka nje, kwa hiyo hawatatuma chochote,"
Bwana Kadyrov mapema aliunga mkono ndoa ya afisa wa Polisi kumwoa msichana wa miaka 17, japokuwa alikuwa tayari ameolewa, katika tukio la ukiukaji wa sheria za Urusi.
Mnadhimu wake wa kijeshi tangu wakati huo alipendekeza kuhalalisha ndoa ya zaidi ya mke mmoja nchini Chechnya.
Bwana Kadyrov, kiongozi wa kimla na mshirika wa karibu wa Rais wa Urusi, Vladimir Putin, katika miaka ya karibuni alipiga marufuku kuwachukua kwa nguvu wanawake kwa ajili ya kufunga nao ndoa za umri mdogo.
Pia anafikiriwa kuwa anapendelea ndoa za wake wengi. Msaidizi wake mkuu Magomed Daudov anasema: "hiyo yote inaendana na Sharia. Lakini kama mwanaume anaweza kuhudumia zaidi ya mke mmoja, kwa nini asioe wengi?" Watu wengi katika jamhuri ya ya Urusi ya Chechnya, ni Waislamu.