MAHAKAMA ya
hakimu mkazi mkoa wa Njombe imetupilia mbali kesi iliyo kuwa inamkabili
mfanyabiashara maarufu mkoani Njombe, Mexons Sanga pamoja na mkewe Happy
Mwasamile na meneja wake jana ya kudaiwa kuzuia maafisa wa Mamlaka ya Mapato
Kanda ya Mbeya kufanya kazi katika kampuni yake ya Mexons Investment Ltd.
Mfanyabiashara
hiyo alidaiwa kutenda kosa hilo kinyume na sheria ya kodi namba 4 ya mwaka
2004, sura ya 332 na sura 107, mahakama ya hakimu mkazi jana mbele ya hakimu
Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Njombe, Augustino Rwizile, aliifutilia mbali kesi hiyo
baada ya upande wa serikali kushindwa kuleta faili la mashitaka pamoja na
ushahidi.
Wafanyabiashara
mkoani Njombe kwa pamoja walikusanyika mahakamani huku maduka yao yakiwa
yamefungwa kwa masaa 6 kwa lengo la kwenda kusikiliza kesi ya mfanyabiashara
mwenzao.
Wakili wa
serikali akitoa maelezo mbele ya hakimu Rwizile, Wakili Yahaya Misango aliiomba
mahakama iahirishe kesi hiyo kwa mara ya
nne na kupangiwa siku nyingine kwa lengo la kuwasirisha faili la kesi dhidi ya
mshitakiwa.
“Naomba
kesi hii ipangiwe siku nyingine kwa kuwa wakili alikuwa anatoka Mbeya,
hajatuletea vielelezo vya kesi kutoka ofisi ya Mbeya,” alisema Misango.
Kutokana na
kesi hiyo kuto endeshwa kwa zaidi ya siku mbili Hakimu Rwezile alisema ameifuta
kesi hiyo kwa kutumia kifungu cha 225 kifungu kidogo cha 5 baada ya kushindwa
kuleta ushahidi dhidi ya mshitakiwa mahakamani.
Aidha kwa
upande wake wakili wa Mwxsons akingumzia kufutwa kwa kesi dhidi ya mteja wake
nje ya mahakama hiyo, Wakili Daniel Welwel alisema hakimu ameamua kuifuta kesi
hiyo kufuatia washitaki ambao ni Jamhuri kwa mara tatu mfululizo kushindwa kuendesha kesi hiyo.
Naye
mshitakiwa Mexons akizungumza mara baada ya kufutiwa kesi hiyo, alisema
anaishukuru mahakama kwa kutenda haki.
Mnamo
Februari 8, mwaka huu mshitakiwa Mexons alifikishwa mahakamani na TRA kwa
kudaiwa kutenda kosa la kuwazuia kufanya kazi maofisa wa TRA, Februari 3 katika
ofisi yake.
Awali
mwanasheria wa TRA Nyanda za Juu Kusini, Juma Kisongo akisoma kesi hiyo mnamo
Februari 8, alisema mtuhumiwa alifikishwa mahakamani hapo kwa kosa la kuwazuia
wafanyakazi wa TRA kufanya kazi zao kinyume na sheria.