Wananchi wamkataa mwenyekiti wa mtaa

WAKAZI wa Kijiji cha Madilu Tarafa ya Liganga Halmashauri ya Ludewa Mkoani, wamemkataa Mwenyekiti Mpya wa Kijiji hicho Benito Mgina kwa madai kuwa wao hawakushiriki kumchagua bali alichaguliwa na chama chake cha Mapinduzi (CCM).

Wananchi hao wanamtuhumu Mwenyekiti huyo kuwa aliwahi kughushi sahihi ya mtu kutaka kutumia sh. 200,000 wakati akiwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Matundu inagawa alizirudisha baada ya serikali ya kijiji kumhoji, hivyo wakazi wa kijiji hicho wanahoji kama alitaka kutumia fedha za kitongoji kwa maslahi yake binafsi itakuwaje kama watampa mamlaka makubwa ya kuongoza kijiji.

Wakizungumza katika mkutano wa hadhara wa kijiji wa kukabidhiana ofisi ya kijiji baina ya mwenyekiti huyo wa sasa na wa zamani Deocara Mbwilo, wananchi hao walizuia makabidhiano wakisema kama wangempigia kura ya ndio au hapana na kupita wangekubali akabidhiwe lakini kwa kuwa serikali haikuwapa fursa ya kumpigia kura ndio au hapa licha ya kuwa hakuwa na mpinzani hawamtambui.

“Mnamkabidhi huyo ofisi alichaguliwa na nani wakati sisi hatukumpigia kura? Hatutaki sisi huyo awe mwenyekiti wetu,” alisema Benedict Mbogo

Mbogo alipofuatwa na Mwandishi wa habari hii ili kutolea ufafanuzi sababu zinazopelekea wamkutae mwenyekiti huyo alise: “Huyu mwenyekiti hatumtaki kwa sababu ni mhujumu wakati akiwa Mwenyekiti wa Kitongoji cha Matundu aligushi sahihi ya mtu kutaka kuiba fedha ya umma sasa tukimpa mamlaka makubwa ya kuongoza kijiji itakuwaje? Kwanza hata kupita walimpitisha kiunjanja tu wakati wa kura za maoni ndani ya CCM na sisi wananchi wakati wa kura ya maoni hatukupewa fura ya kumpigia kura ya ndio au hapana ndio maana wananchi hawamtaki”.

Leonard Mwaliongo mkazi wa kijiji hicho alisema: Mimi ninachoelewa kama mgombea yuko peke yake huwa wanaweka picha na kivuli ili wananchi wapige kura aidha wapigie kivuli au mgombea lakini hapa haikufanyika. Walichofanya siyo sahihi maana walipompitisha tu ndani ya CCM wakasema ni Mwenyekiti sasa amepigiwa kura na mwananchi gain zaidi ya wana-CCM”.

Kitendo hicho kilipelekea wananchi hao kumchagua Mwenyekiti wa Kitongoji Cha Madilu Protas Mtega kuwa Mwenyekiti wa muda na hivyo kukabidhiwa ofisi pamoja nna mali za kiji na mwenyekiti wa zamani.

Akizungumzia tukio hilo Mwenyekiti wa zamani wa Kijiji hicho ambaye pia ni Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Liganga Deocara Mbwilo, alikiri Mwenyekiti huyo kukabiliwa na tuhuma za hizo, kwa kusema kuwa wananchi wanachukulia hicho kama kigezo cha kumkataa lakini fedha hizo ambazo zilikuwa na matatizo katika hesabu za kitongoji alishazirudisha.
 
Mtendaji wa Kijiji hicho Boniface Sikalila, alisema kama wananchi hao hawamtaki Mwenyekiti huyo wanapswa kuandika barua kwenda kwa msimamizi wa uchaguzi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ludewa ili aweze kuwapa muongozo lakini yeye hana mamlaka kwa mujibu wa sheria.


Juzi ilikuwa mara ya pili kwa wananchi hao kukataa kwa Mwenyekiti huyo kukabidhiwa ofisi ya kijiji na mali za kijiji, kufuatia kumkataa tena katika mkutano wa kumkabidhi wa Februari 4, mwaka huu ambao ulivunjika kwa vurugu, na kupelekea baadhi ya vijana wa kijiji hicho kukamatwa na polisi kwa ku tuhuma za kuvuruga mkutano.