DRFA YAIPA MBINU YANGA KUINYOA ETOILE DU SAHEL
Kuelekea mchezo wa michuano ya kombe la shirikisho barani afrika kati ya Yanga dhidi ya Etoile Du Sahel ya Tunisia utakaopigwa jumamosi hii April 18 katika uwanja wa taifa,Chama cha soka mkoa wa Dar es salaam DRFA,kimeitabiria makubwa klabu hiyo ya Jangwani kuvuka katika kizingiti hicho kigumu kwa mchezo wa nyumbani na ugenini dhidi ya wababe hao wa Tunisia.
Mwenyekiti wa chama hicho Almasi Kasongo,amesema ili yanga ifanye vizuri katika mechi hiyo na kuwapa raha mashabiki wake na watanzania kwa ujumla,ni lazima icheze kwa uangalifu mkubwa na kukwepa kuendana na style ya kupoozesha mpira wanayoitumia wapinzani katika mechi za ugenini.
kasongo amelishauri benchi la ufundi la Yanga chini ya makocha Hans Pluijm na msaidizi wake Charles Mkwasa,kutumia mbinu ya kushambulia kwa muda wote ili kuwaduwaza wapinzani ambao wakati mwingine hutumia mbinu ya kufanya mashambulizi ya kushtukiza.
Ametoa wito pia kwa mashabiki wa soka mkoa wa Dar es salaam na maeneo ya jirani, kujitokeza kwa wingi siku ya jumamosi kuishangilia Yanga ambao wanaliwakilisha taifa katika mashindano hayo ya vilabu barani afrika.
Hata hivyo DRFA inaamini kuwa Yanga ambayo ni moja ya timu zake zilizopo katika mkoa wa Dar es salaam haina sababu ya kutofanya vizuri katika mchezo huo, kutokana na kuwa na kikosi kizuri kilichovisambaratisha katika michuano hiyo vilabu vya BDF ya Botswana pamoja na Platinum ya Zimbabwe.
KILA LA KHERI YANGA JUMAMOSI
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini TFF, Jamal Malinzi ameitakia kila la kheri timu ya Young Africans katika mchezo wake wa jumamosi wa Kombe la Shirikisho barani Afrika (CC) dhidi ya timu ya Etoile du Sahel kutoka Tunisia, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Katika salamu zake kwa klabu ya Young Africans, Rais Malinzi amewaambia wanapaswa kupambana na kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo wa jumamosi, ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele katika mchezo wa marudiano kwani ndio pekee kwa sasa wanaoipeperusha bendera ya Tanzania katika michuano ya kimataifa.
Young Africans imeingia katika hatua ya 16 bora Kombe l Shirikisho barani Afrika,baada ya kuzitoa BDF XI ya Botswana katika hatua ya awali kwa jumla ya mabao (3-2), kisha kuwaondoa FC Platinum ya Zimbabwe katika hatua ya kwanza kwa jumla ya mabao (5-2).
Endapo timu ya Young Africans itafanikiwa kuwaondoa Etoile du Sahel itasuburia kucheza mechi ya mtoano (Play-off) dhidi ya timu mojawapo zitakaotolewa katika 16 bora ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika (CL).
Wakati huo huo wapinzani wa Young Africans timu ya Etoile du Sahel wanatarajiwa kuwasili saa 9 usiku kuamkia ijumaa kwa usafiri wa Ndege ya kukodi ya kampuni ya Nouvelair bj 4870 wakiwa na msafara wa watu 56.
Makamu wa Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Tunisia (FTF), Bw. Krifa Jalel ndiye mkuu wa msafara huo akiwa na Rais wa klabu ya Etoile du Sahel (ESS) Bw.Charefeddine Ridha, wachezaji 19, benchi la ufundi lenye watu 13, waandishi wa habari 12 na wanachama 10
Timu ya Etoile du Sahel itafikia katika hoteli ya Ledger Plaza zamani Bahari Beach eneo la Kunduchi, na kesho jioni ijumaa wanatarajiwa kufanya mazoezi katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Waamuzi wa mchezo huo ni Samwel Chirindiza, Arsenio Marenguka, Celio de Jesus Musabe, Jose Maria Bachide wote kutoka nchini Msumbuji na wanatarajiwa kuwasili leo mchana, huku kamisaa wa mchezo huo Salah Ahmed Mohamed kutokea nchini Sudan akitarajiwa kuwasili leo jioni na wote watafikia katika hoteli ya Protea iliyopo Oysterbay.