WAZEE WAMTAKA FILIKUNJOMBE ACHUKUE FOMU


Baadhi ya wazee wilayani Ludewa wamemuomba Mbunge wa Jimbo la Ludewa, Deo Filikunjombe kuchukua fomu ya kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu mwaka huu na kudai wamechoshwa na tabia ya kubadilisha viongozi.
Wakizungumza mjini hapa wakati wa sherehe za miaka 38 ya kuzaliwa Chama cha Mapinduzi (CCM)iliyofanyika kijiji cha Nsele Kata ya Kilondo wilayani Ludewa, wazee hao wamewataka wananchi katika jimbo la Ludewa kuendelea kumuamini mbunge huyo, kwani hawaoni sababu ya kumbadili kiongozi ambaye bado wanaimani naye ya kuendelea kuwaongoza.
Mwanasiasa mkongwe wilayani hapa ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ludewa, Mzee Hilali Nkwera alisema kuwa ni tabia iliyozoeleka kwa wananchi kubadili viongozi kila kinapofika kipindi cha uchaguzi hali ambayo inarudisha maendeleo ya wilaya nyuma.
“Katika historia ya wilaya ya Ludewa ni mbunge mmoja pekee ndiye aliyewahi kudumu madarakani kwa muda wa miaka 25 ambaye ni hayati Mathias Kihaule, lakini tangu alipochukua utawala huo hayati Horace Kolimba (aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi) imekuwa ni desturi ya kubadilishana kila kipindi, hali ambayo ni mbaya kwa maendeleo kwani mikakati ya kimaendeleo haiwezi kufanikiwa kwa muda wa miaka mitano,” alisema Nkwera.
Alisema mbunge Filikunjombe ameanza kufanya maendeleo kwa kasi kubwa hivi sasa katika jimbo lake na wilaya ya Ludewa kwa ujumla, hivyo hapaswi kupingwa zaidi ya kuungwa mkono kwa yale anayoyafanya kwani wananchi wa wilaya ya Ludewa hawana haja na mtu mwingine wa kuliongoza jimbo hilo.
 “Sisi kama wazee wa wilaya ya Ludewa hatuna haja ya mbunge mwingine, wako vijana wanaokuja kutuomba tuwape nafasi na tumewajibu wamuache mwenzao aendelee na mipango aliyoianza kuitekeleza ili wilaya ibadilike zaidi tofauti na zamani, tumeamua kuacha tabia ya kubadilisha wabunge kila mwaka kwani tumeziona athari zake za kurudi nyuma kimaendeleo”, alisema Nkwera.
Akiunga mkono kuhusu ombi la kutaka wananchi wawe na imani na Filikunjombe,  Bi.Gerewada Nyandoa alisema kwa upande wa wakina mama katika wilaya hiyo hawanashida na utendaji kazi wa Filikunjombe, ambapo alisema ameweza kuwasaidia katika maendeleo ya ujenzi wa Zahanati ambazo ni mkombozi kwa mwanamke hivi sasa katika wilaya hiyo.
“Kabla ya ujenzi wa Zahanati, sisi wanawake tulikuwa tukipata taabu wakati wa kwenda kupata matibabu, lakini toka alipochaguliwa mbunge Filikunjombe, jumla ya Zahanati tatu zimeshakamilika na zinatoa huduma, hili ni jambo la kumpongeza mbunge, tulikuwa tunatembea umbali mrefu kufuata matibabu,” alisema Nyandoa.
Alisema hivi karibuni wazee wa kijiji cha Nsele Kata ya Kilondo walitoa fedha shilingi laki moja na kumkabidhi Filikunjombe ili aweze kujiandaa kuchukua fomu ya kugombea ubunge kwenye jimbo la Ludewa.
Kwa upande wake, Mzee George Kilongo anayewakilisha wazee waliopo mwambao wa Ziwa Nyasa aliusifia uongozi wa mbunge huyo katika kuwaletea maendeleo wananchi wake, kwani ameweza kutembelea vijiji vyake vyote vya Ziwa Nyasa ndani ya miaka mitano licha ya kuwa na Jiografia yenye milima na mabonde, lakini mbunge huyo ameweza kufika vijiji vyote 77.

“Mfano  vijiji  vyenye mazingira magumu ya kufikika ni kijiji cha Liunji,Kimata na Nkwimbili ambako hakuna mbunge ambaye aliwahi kufika, lakini Filikunjombe ameweza kuvitembelea na kutoa misaada ya Afya,Elimu na maji hali ambayo imewafanya wananchi wa vijiji hivyo kuona kuwa mbunge huyo anapaswa kuendelea kuiongoza wilaya ya Ludewa kwa muda mrefu ili kuendelea kuwasaidia wananchi,” alisema Kilongo.

Na Nyanda za Juu blog