Yote Uliyowahi Kutaka Kujua Kuhusu Mkito.com: Mahojiano ya Bongo Celebrity na Mwanzilishi Mwenza,Sune Mushendwa


Sune Mushendwa-Mkito.com  
Sune Mushendwa

Kwa miaka nenda rudi, wasanii wa kitanzania walikuwa na kilio kinachofanana. Ungekaa pembeni bila kuwaona, ungedhani kutokana na mwangwi wa kilio chao, anayelia ni mmoja. Hapana. Wote walikuwa [na pengine bado wanaendelea kulia] kutokana na kunyonywa “jasho lao”. Kimsingi “jasho” wanalolilia limekuwa ni soko na usambazaji. Kipaji unacho na watu wanakubali kazi zako. 
Tatizo utaifikishaje kazi yako kwa mashabiki zako? Ni wazi kwamba unahitaji msaada wa kimasoko na usambazaji. Kusema utaweza kufanya kila kitu peke yako ni kujidanganya.Nani? Yupo wapi na utampa kazi zako kwa thamani gani? Kilio chao kilianzia hapo. 
Wengine wakaamua kuachana na muziki [wengine muziki umewaacha wao] kutokana na ukosefu wa soko la uhakika na kuona kadhaa ya kupanga foleni ukisubiri “hela yako”. 
 Mabadiliko ya masoko ya kazi za wasanii duniani kutoka kwenye mifumo ya ki-analojia kwenda kwenye dijitali na pia kutoka katika mifumo ya vitu kama CD mpaka kwenda kwenye matumizi ya simu na vikabrasha vingine vya mikononi, kulimaanisha kwamba soko la wasanii wa kitanzania [na Afrika kwa upana wake] lilikuwa linazidi kufifia. Hakuna tena shabiki anayetaka kubeba furushi la CD. Inakuwaje? 
 Hapo ndipo baadhi ya vijana wakaona fursa kuthibitisha kwamba penye tatizo ndipo pa kukimbilia.Fursa ni kama dhahabu au almasi.Huwezi kuiokota kando ya bahari ikiwa imetupwa ufukweni na mawimbi ya bahari. Wazo la fursa likazaa Mkito.Com mahali ambapo wasanii sasa wanapumua na huku changamoto pekee ni kuwashawishi mashabiki kupakua kazi zao kutoka Mkito.Com. Kila mara shabiki anapofanya hivyo, msanii ananufaika na kupata nguvu zaidi ya kuingia tena studio kunogesha mambo. 
It’s a win win situation.   Sune Mushendwa [pichani juu] ni mwanzilishi-mwenza wa Mkito.Com. 
Kujua mengi zaidi nilimtafuta na kupiga naye story kidogo. Ameelezea mengi. Nakukaribisha usome mahojiano yangu naye ili ujue yote ambayo umekuwa ukitaka kuyajua kuhusu Mkito.Com .Twende pamoja;   

BC: Sune karibu sana ndani ya BongoCelebrity. Hii ni mara yako ya kwanza hapa na bila shaka wasomaji wangependa kupata japo kwa kifupi tu historia yako. Ulizaliwa wapi,ukakulia wapi na kusomea wapi na mambo kama hayo? 

SM: Asante sana kwa kunikaribisha. Mimi nimekulia Arusha na ndipo niliposoma pia. Baada ya sekondari nilienda kusoma chuo kikuu nchini Finland ambako mama yangu ndipo anapotokea. 

BC: Wajasiriamali wengi ambao nimewahi kufanya nao mahojiano huniambia kwamba waliamua kufanya wanachokifanya baada ya kukosa au kubughudhiwa na kitu fulani.Huwa kuna kisa au mkasa nyuma ya pazia. Kwa upande wa Mkito kuna kisa au mkasa wowote? Ilikuwaje mpaka ukasema Aha…Mkito ikaanza? Na hili jina lilikuja namna gani?  

SM: Baada ya kutoka masomoni nilianzisha studio ya muziki Arusha.Lakini tatizo kubwa lililoonekana moja kwa moja ni kwamba wasanii pamoja na studio zinapata tabu sana katika kusambaza na kuuza kazi zao. Niliona tunahitajika njia ya kuweza kusambaza muziki kirahisi na pia kuingiza kipato kwa msanii. Baada ya research na maandalizi ya zaidi ya miaka 4 ndipo Mkito.com ilipozaliwa tarehe 30 April 2014. 

BC: Mpaka sasa Mkito imefanikiwa kuwa na wasanii wangapi? Nini masharti ya msanii kujiunga au kuweka kazi zake katika Mkito?   
SM: Kuna wasanii takriban 600 waliojiunga mpaka sasa na wanaongezeka kila siku. Masharti ya kujiunga ni marahisi, uwe umerekodi wimbo anghalau mmoja wenye ubora. Baada ya hapo msanii anaweza kujitengenezea akaunti yake kupitia tovutiwww.mkito.com na kupakia[upload] nyimbo zake mwenyewe. Msanii baada ya hapo anaweza kufuatilia mauzo yake mwenyewe kupitia akaunti yake aliyoitengeneza.   

BC: Bado nikiwa katika swali au maswali ya wasanii. Msanii akishaingia katika mkataba au makubaliano na ninyi, bado anakuwa na haki na uhuru wa kuendelea kusambaza kazi zake katika platforms zingine kama vile iTunes,Spotify,Google Play nk?
  SM: Tunaamini kuwa kazi ya msanii ni mali yake pekee kwahivyo hatumzuii msanii aliyejiunga nasi kusambaza kazi zake kwa njia yoyote nyingine aipendayo. Kama huduma yetu ni bora basi tunaimani msanii mweyewe atachagua kutumia huduma zetu siyo mpaka tumfunge kupitia mikataba.  

BC: Nilisoma mahali kwamba mlipoanzisha Mkito lengo lilikuwa kuwa na watumiaji waliojiandikisha [registered users] milioni 1 katika mwaka wa kwanza. Mpaka sasa mmefikia wapi katika lengo hilo?   SM: Nilishasoma hilo mimi pia lakini siyo ukweli kuwa lengo ni kufikisha watumiaji milioni 1. Lengo ni kufikisha watumiaji waliyojiandikisha laki 5 ndani ya mwaka moja. Tumekaribia nusu ya hiyo idadi mpaka sasa na dalili zote ni kuwa tutafika na kuvuka hiyo idadi.   

BC: Kuna baadhi ya wasanii ambao nimeongea nao kuhusu huduma kama hii ya Mkito na nyinginezo wanasema kwamba huduma hizi kimsingi zinawapunja au kuwadhulumu kwa sababu hamuendi nao bega kwa bega katika matayarisho ya muziki [kwa maana ya gharama na karaha zote za maandalizi] bali nyie mnasubiri wapike kisha muwasaidie tu kupakua huku nanyi mkijitengenezea faida. Unawaambiaje wasanii kama hao na kuna tofauti gani kubwa kati ya wasambazaji wale wa zamani na nyie hapo?   

SM: Mkito.com ni kampuni ya usambazaji wa muziki na siyo studio ya kurekodi au kampuni ya management. Kwa maana hiyo sisi faida tunaingiza katika uuzaji wa muziki kupitia tovuti yetu tu. Kama tungehusika na kurekodi na management ya wasanii basi tungedai makato kwenye mauzo yote kama ring tones, CD, shows n.k. lakini kama nilivyosema faida yetu ni katika uuzaji wa muziki tu. Kuhusiana na tofauti ya Mkito.com na makampuni mengine; tangia mwanzo tumehakikisha kuwa mauzo yote yanawekwa wazi ili msanii ajue muda wote kuwa mauzo yake yakoje. Hili bado sijaona likifanyika na wengine ingawa ni la muhimu sana. Inabidi kujiuliza madhumuni ya haya makampuni kutokuweka mauzo wazi.Mkito  

BC: Kwa mtu ambaye hajui Mkito ni nini na angependa kufahamu zaidi na hata kujiunga na huduma ya Mkito[nazungumzia mtu mtumiaji wa kawaida] ungempa maelezo gani kwamba Mkito ni nini na nini ategemee pindi atakapoingia Mkito.com?   
SM: Mkito.com ni huduma ya kwanza nchini ya kusambaza muziki kidigitali ambapo mtu anaweza kupakua nyimbo kwa sh 250 tu kupita simu yake au computer. Pia nyimbo zote zinapatikana bure lakini zinaambatanishwa na matangazo mafupi ya kibiashara. Haya matangazo katika nyimbo za bure ndiyo yanawalipa wasanii. Ni muhimu kujua kwa Watanzania wote kuwa ni jukumu letu kulinda muziki wetu na unavyopakua nyimbo kupitia Mkito.com unakuwa unauhakikia kuwa msanii analipwa kwa kazi yake na wewe pia unasaidia kuuendeleza muziki wa Kitanzania.   
BC: Bila shaka kwenye biashara kama ya Mkito ambayo kwa ukaribu sana inahusiana na tekinolojia za mitandaoni,matatizo hujitokeza.Kuna mtu kushindwa kupakua[download] wimbo au nyimbo na kuna kero zingine nyingi.Mkito mnashughulikiaje matatizo kama hayo? Na kimsingi ni changamoto gani ambazo mnakabiliana nazo kila siku au mara kwa mara?  

SM: Kuna maelfu ya aina tofauti za simu na computer ambazo kila siku zinatumika kupakua nyimbo Mkito.com. Sasa ni vigumu kuhakikisha kuwa tovuti itafanya kazi na kila aina ya simu lakini kwa kiasi kikubwa sana tumefanikiwa kutatua matatizo yanapojitokeza. Pia tunayo huduma kwa wateja ili mtu akipata shida anaweza kutuandika barua pepe au kupiga simu na tunamsaidia kutatua tatizo lake haraka.   

BC: Kwa upande wa muziki, wasanii,wasimamizi [managers] wao nk nikikupa nafasi hii kuongea nao moja kwa moja ungewaambia nini au ungewapa ushauri gani kuhusiana na suala zima la muziki nk?   

SM: Muziki ni biashara, wote tunafahamu hilo. Kwahiyo ninawakaribisha wasanii wote kuja kujiunga Mkito.com tuwasaidie kutangaza, kusambaza na kuuza muziki wao. Nafahamu kuwa wengi wanakuwa na wasiwasi kuwa wataibiwa – hili siyo kweli kwa upande wa Mkito.com, labda waliotutangulia. Kama nilivyokwisha sema kila kitu kinawekwa wazi na kama wewe ni msanii mwenye kazi nzuri basi kuwa na imani kuwa unaweza kujipatia kipato kizuri kutokana na mauzo ya muziki wako kupitia Mkito.com   

BC: Shukrani sana kwa muda wako Sune. Nakutakia kila la kheri katika kazi zako   Asante sana. Lakini na mimi nikuulize wewe swali moja. Je, umeshapakua nyimbo ngapi mpaka sasa kupitia Mkito.com ili kuwapa support wasanii wa Tanzania? J 

BC: Mpaka leo,nimeshapakua nyingi.Sikumbuki idadi kamili. Lakini mchango wangu zaidi ni kuwajulisha watumiaji wengine [wasomaji wangu kwa mfano] juu ya kazi mpya za wasanii na wapi pa kuzipata.

 Asante kwa swali zuri Sune.