Jeshi la polisi nchini linawashikilia vijana 36 wa kundi maarufu Panya Road wanaodaiwa kufanya vurugu na kupora mali za watu na kusababisha taharuki katika jiji la Dar es salaam huku baadhi ya wananchi wakitoa maoni tofauti kuhusiana na tukio hilo.
Akitoa ufafanuzi wa taharuki hiyo msemaji wa jeshi la polisi SSP ADVERA BULIMBA ambaye mbali na kuwatoa hofu wananchi kuwa hali hiyo haitajitokeza tena amesema jeshi hilo limejipanga vizuri kukabiliana na vikundi vyovyote vinavyotaka kuvuruga amani ya nchi na kwamba endapo polisi wasingewadhibiti vijana hao mapema tangu wakiwa makaburini baada ya kumzika mwenzao aliyeuwawa na wananchi baada ya kuiba hali ingekuwa mbaya zadi.
Kufuatia tukio hilo ITV imezunguka maeneo mbalimbali ya jiji yaliyodaiwa kukumbwa na tafrani hiyo ambapo baadhi ya wananchi wa maeneo ya magomeni ambako vurugu zilianzia wameelezea namna zilivyoanza hadi kusababisha watu kuanza kukimbia hovyo na wengine kuacha maduka yao wazi na taarifa kusambaa maeneo mengine.
Katika maeneo ya mwananyamala na ubungo baadhi ya waliozungumzia sakata hilo wameitaka serikali kuangalia makundi ya vijana na ikiwezekana wapatiwe elimu ya ujasiriamali bure ili waweze kuendesha maisha huku wengine wakishauri vijana wasiokuwa na kazi mitaani wapelekwe jeshini wakafundishwe stadi za kazi pamoja na uzalendo ili kuepuka vitendo hivyo.
Taharuki hiyo ilitokea usiku wa tarehe mbili chanzo kikiwa ni kijana mmoja aliyejulikana kwa jina la MOHAMED AYUB kuuwawa na wananchi tarehe mosi mwaka huu katika maeneo ya tandale kwa mtogole kwa tuhuma za wizi ambapo tarehe 2 maziko yalifanyika na taarifa zilizolifikia jeshi la polisi zilidai kuwa baada ya maziko vijana wenzake walijipanga kufanya fujo ili kulipiza kisasi.
SOURCE: ITV