RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete (Pichani) amefanya uteuzi
wa Makatibu Wakuu wa Wizara kwa kuteua Makatibu Wakuu wanne wapya na kuhamisha
mmoja.
Aidha, Rais Kikwete amefanya uteuzi na
uhamisho wa Makatibu Tawala wa Mikoa.
Taarifa iliyotolewa
mjini Dodoma jioni ya leo, Jumatano, Novemba 5, 2014 na Katibu Mkuu Kiongozi,
Balozi Ombeni Sefue imesema kuwa walioteuliwa kuwa Makatibu Wakuu ni Dkt. Donan
Mmbando ambaye anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt.
Yohana Budeba ambaye anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na
Uvuvi, Mhandisi Mbogo Futakamba kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Dkt.
Adelhelm James Meru ambaye anakuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na
Maliasili.
Kabla ya uteuzi wake,
Dkt Mmbando alikuwa Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Budeba alikuwa Naibu Katibu
Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Uvuvi na Mifugo, Mhandisi Futakamba alikuwa
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maji na Dkt. Meru alikuwa Mkurugenzi Mkuu, Mamlaka
ya Maeneo Maalum ya Uwekezaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA).
Aidha, taarifa hiyo
imesema kuwa Rais Kikwete amemhamisha Bibi Maimuna Tarishi kutoka Wizara ya
Maliasili na Utalii kwenda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria
Kuhusu uteuzi na
uhamisho wa Makatibu Tawala wa Mikoa, Rais Kikwete amemteua Bw. Charles
Pallangyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuwa Katibu Tawala
wa Mkoa wa Geita, Bw. Adoh Steven Mapunda, Mkurugenzi Mtendaji, Manispaa ya
Bukoba kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Bw. Severine Kahitwa, Katibu
Tawala wa Mkoa wa Geita kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro na Dkt.
Faisal Issa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa
Mwanza.
Wakati huo huo, Rais
Kikwete amemteua Kanali (Mst) Joseph Simbakalia, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, kuwa
Mkurugenzi Mkuu wa EPZA.
Uteuzi huo unaanza
leo na Makatibu Wakuu na Makatibu Tawala wa Mikoa wataapishwa kesho, Alhamisi,
Novemba 6, 2014, Ikulu, Dar es Salaam.
Mwisho.
Imetolewa na;
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu – Dar es Salaam.
05
Novemba,2014