Wangin'ombe yapatiwa cheti

MKUU wa mkoa wa Njombe hivi karibuni ameutoa utata wa makao makuu ya wilaya ya Wanging’ombe baada ya kukabidhi cheti kinacho onyesha makao makuu ya wilaya hiyo yenye mwaka mmoja.

Kapteni Mstaafu Asseri Msangi alikabidhi cheti hicho mwishoni mwa wiki iliyo pita katika naraza la madiwani wa halmashauri ya wanging’ombe ambacho kinachoonyesha makao makuu ya Wilaya hiyo ikiwa ni mwaka mmoja tangu kuanzishwa na kimetoa kauli ya serikali inayoondoa utata wa makao makuu.

Awali cheti hicho kilikosewa uchapaji na kuto onyesha eneo maalamu la kujengwa kwa makao makuu, ambapo kilionyesha  makao makuu yalitakiwa kuwepo Wanging'ombe  badala ya Igwachanya yaliposasa na kusababisha kuibuka kwa mvutano juu ya sehemu sahihi  ya makao makuu ya wilaya hiyo licha ya kutangazwa na serikali.


Msangi  alipokuwa akikabidhi cheti hicho, aliwataka watendaji wa halmashauri hiyo kupanga mipango yake vema kwani cheti wameshakipata ambacho kinaonyesha uhalali wa wilaya hiyo na kuacha malumbano ya kisiasa.


"Kuna waliotaka iwe wangin'gombe  wengine iwe Igwachanya na wengine walitaka iwe Mdandu, lakini mwenye uamuzi wa mwisho ni Katibu Tawala wa Mkoa (Ras) kwa mujibu wa sheria kwenye gazeti la serikali la mwezi April mwaka jana  lilitangaza kuanzishwa kwa halmashauri 19 ikiwemo hii ya kwenu" alisema Msangi


Aliongeza; "Kwa bahati mbaya spika wa bunge alikosea kuandika jina la makao makuu itakuwa wangin'gommbe imetuchukua muda mrefu kufuatilia lakini hatimaye tumefanikiwa na leo nimekuja rasmi kuwakabidhi cheti chenu."

Msangi aliwataka viongozi hao kuitumia fursa hiyo kama chachu ya kuupanga vizuri mji huo ikiwa ni pamoja na kuweza majengo katika mpangilio ambao utaufanya mji kuonekana wa tofauti.

"Kazi ni kwako mtu wa mipango miji tusifanye kosa kama walivyofanya wenzetu kwenye miji mingine hapa nchini, tufanye kitu ambacho kitakuwa tunu kwa wananchi ambao watakuja kuishi miaka mingi ijayo," alisema Msangi.

Kwa Upande wake Kamanda wa Tume ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Njombe Charles Nakembetwa  aliwataka watumishi wa halmashauri hiyo kuongeza bidii katika shughuli za maendeleo bila ya kuhusiha masuala ya Rushwa.


Hivyo aliwataka kuzingatia utumishi bila ya kuendekeza kupokea Rushwa ili kuiweka halmashauri katika muonekani mzuri na kuwavutia wananchi kutoka sehemu mbalimbali za halmashauri hiyo kenda kupata huduma.

Naye Mwenyekiti wa  Halmashauri ya Wilaya ya Wanging'ombe Antony Mahwata alimuahidi Mkuu wa Mkoa kuwa  wataendelea kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kuishukuru ofisi ya mkuu wa mkoa kwa juhudi walizozifanya hadi kupatikana kwa cheti hicho.


"Kwa niaba  ya wenzangu tunashukuru serikali ikishasema hilo ni agizo tunatakiwa kulitekeleza  tutahakikisha kila kitu kinajengwa kwa kiwango  kinachotakiwa na tunashukuru pia kupata cheti ambacho kinaonyesha uhalali wa Halmashauri yetu" alisema Mahwata.