Marufuku ya kubusiana kwa wanafunzi ZIM


Chuo Kikuu cha Zimbabwe chapiga marufuku kubusiana au kukumbatiana
Amri iliyowekwa na Chuo Kikuu cha Zimbabwe ya kuwazuia wanafunzi kubusiana imeelezwa kuwa haina "mantiki", mwakilishi wa wanafunzi ameiambia BBC.
Agizo kutoka mamlaka ya chuo kikuu imesema "ukikutwa katika mkao wa kubusiana" katika kampasi ya Harare utaadhibiwa.
"Katika umri huu tuseme siruhusiwi kubusu au kumkumbatia mtu... ni kukosa akili," Tsitsi Mazikana amesema.
Uongozi wa chuo kikuu haujasema lolote kuhusu hatua ya wanafuzni kupinga amri hiyo.
Amri hiyo ilitolewa mwanzoni mwa mwaka wa masomo kama sehemu ya orodha ya vitendo vya utovu wa nidhamu ambavyo vinahitaji hatua za haraka kuchukuliwa kutoka mabweni ya wanafunzi".
Sheria ya chuo kikuu cha Zimbabwe inaorodhesha mambo 11 ambayo ni "utovu wa nidhamu" ambayo yatawezesha mwanafunzi kufukuzwa chuo.
Katika orodha hiyo ya mambo 11 pia inapiga marufuku msongamano na kupika katika vyumba vya kulala.
Miongoni mwa amri za chuo kikuu cha Zimbabwe
Jambo la nne katika tabia ambalo litamlazimisha mwanafunzi kufukuzwa linasema: "kukutwa katika mkao wenye kuonyesha kubusiana au kufanya mapenzi hadharani".
Bi Mazikana, ambaye ni mwanafunzi mwakilishi wa jinsia, amesema kuwa kampasi tayari ina sheria ngumu kwa wale ambao wanashirikiana na jinsia nyingine.
Katika hosteli za mtu mmoja mmoja, kwa mfano, wakaazi wake wanaruhusiwa kuwapokea wageni wao na kuishia sebuleni na wageni hawaruhusiwi kufika katika hoteli hizo baada ya saa Nne usiku, amesema.
Bi Mazikana amesema amri hiyo haina chochote kuhusiana na maadili na zaidi ya hapo ni kuwadhibiti tu wanafunzi ambao"hawafurahii namna chuo kikuu hicho kinavyoendeshwa".
"kama walikuwa wakichukulia kila kitu kuwa ni cha kimaadili wasingeweka kondom katika hosteli na katika zahanati, lakini... kubusiana na kukumbatiana - hakuna kitu kisicho cha maadili hapo," ameiambia BBC.
Chama cha wanafunzi nchini Zimbabwe (Zinasu) amesema utawala wa chuo kikuu umekuwa na tabia ya kuweka sheria zenye utata bila kushauriana na vyombo vya wanafunzi.
Umoja wa wanafunzi wanaandaa pingamizi dhidi ya sheria inayozuia kubusiana, kiongozi wa chama cha wanafunzi, Zinasu, Gift Maposa amekiambia kipindi cha BBC cha Focus on Africa.
Tayari kumekuwa na sheria zinazoingilia haki za wanafunzi kuandamana- iliyoanzishwa mwaka 1997 - ambayo imechochea hofu miongoni mwa wanafunzi kufukuzwa.
Mwandishi wa BBC, Brian Hungwe kutoka mji mkuu, Harare, anasema wanafunzidaima wanaushutumu utawala wa chuo kikuu kwa kujiweka mbali na fikra za vijana.
Kinywaji cha bia kilipigwa marufuku katika kampasi miaka saba iliyopita, sheria ambayo imepuuzwa kwa kiasi kikubwa.