Muungano unaoongozwa na Marekani
dhidi ya kundi la dola la kiislamu IS umefanya mashambulizi mapya ya
kutokea angani dhidi ya kundi hilo nchini Syria, yaliyolenga viwanda vya
mafuta kwa siku ya pili
Shirika la kutetea haki za binaadamu la Syria
limeripoti kutokea mashambulizi mapya katika mkoa wa mashariki mwa
Syria wenye utajiri wa mafuta, Deir Ezzor, na Hasakeh katika upande wa
kaskazini mashariki, maeneo ambayo pia yalishambuliwa siku moja kabla.
Mashambulizi yote ya
kutokea angani yalivilenga visima vya mafuta katika mikoa hiyo miwili,
ambako wanamgambo wa IS huchukua mafuta yao kwa ajili ya biashara ya
magendo.
Watalaamu wanasema kuwa mauzo ya mafuta kutoka Syria na Iraq ni miongoni
mwa chanzo kikubwa cha mapato ya kundi hilo, ambalo hutengeneza karibu
dola milioni moja na tatu kwa siku.
Wakati huo huo nchini Uingereza wabunge wanajiandaa kupiga kura
ya kuamua kama nchi hiyo itajiunga na operesheni ya mashambulizi ya
kutokea angani dhidi ya kundi hilo nchini Iraq, ijapokuwa hakuna
uwezekano wa Uingereza kushiriki katika mashambulizi yanayofanywa nchini
Syria.
Waziri Mkuu wa uingereza David Cameron akiuhutubia mkutano wa kilele mjini New York
kabla ya kurejea nyumbani alisema lazima juhudi za pamoja zichukuliwe
ili kuukabili ugaidi. Kama bunge la Uingereza litaidhinishisha nchi hiyo
kujiunga na mashambulizi, ndege za kivita za Jeshi la Uingereza
zitajiunga na ndege za Marekani, Ufaransa, Saudi Arabia, Umoja wa Falme
za Kiarabu, Bahrain na Jordan katika kuzipiga ngome za IS. Tayari Baraza
la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha azimio la kupambana na
wapiganaji wa kigeni.
Ubelgiji na Uholanzi pia zinapanga kutuma ndege za kurusha mabomu aina
ya F16 ili kujiunga na operesheni ya Iraq. Uholanzi pia itatuma
wanajeshi 250 pamoja na maafisa wengine 130 wa kutoa mafunzo kwa jeshi
la Iraq wakati naoy Ugiriki ikisema itatuma silaha kwa wanajeshi wa
Kikurdi wanaopambana na majihadi.
Hapo jana, polisi jijini London
iliwakamata watu tisa wanaoshukiwa kuwa na mahusiano na wanamgambo
wenye itikadi kali za kiislamu, akiwemo mhubiri mmoja mwenye msimamo
mkali.
Nalo shirika la ujasusi la Marekani FBI limesema limemtambua mwanamgambo wa Dola la Kiislamu
aliyeonekana katika video zinazoonesha wanahabari wawili wa Marekani
wakichinjwa na mfanyakazi wa misaada wa Uingereza, ijapokuwa limekataa
kutoa maelezo zaidi. Mashambulizi ya kutokea angani yanayofanywa na
majeshi ya muungano nchini Syria yameripotiwa kuwauwa karibu wapiganaji
140 pamoja na raia 13, ijapokuwa wizara ya ulinzi ya Marekani imesema
bado inachunguza ripoti za kuwepo vifo vya raia.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Subscribe to:
Post Comments (Atom)